Makala

MAPITIO YA TUNGO: Masaibu Mbugani; Hadithi kuhusu utunzaji mazingira kwa ubunifu wa kipekee

June 5th, 2019 2 min read

Jina la utungo: Masaibu Mbugani

Mwandishi: Ngulamu Mwaviro

Mchapishaji: Kenya Literature Bureau

Mhakiki: Nyariki E. Nyariki

Kitabu: Hadithi ya watoto

Kurasa: 90

MAMBO mawili yanaipa simulizi hii mvuto wa kipekee.

Kwanza, ni mandhari ya usimulizi.

Kisa kinazunguka mandhari yanayonata fikira za rika lengwa hasa lile la wanafunzi wa madarasa ya juu katika shule za msingi. Hadithi inaanzia jijini katika mtaa wa Donholm.

Ngulamu Mwaviro anaichangamanisha likizo ndefu ya muhula wa tatu na shughuli ambazo zinaipa likizo yenyewe uhai wa pekee na kuondolea mbali kimwa ambacho aghalabu huandamana na likizo za aina hiyo.

Mojawapo ya shughuli hizo jinsi zinavyojitokeza mwanzomwanzo mwa hadithi hii ni mashindano ya michezo ya mitaani hasa mchezo wa kandanda. Tena kuna ziara ambazo zinapendwa sana na rika lengwa.

Usimulizi huu unatupeleka mpaka kijiji kidogo kiitwacho Ngonyi katika wilaya ya Taveta kisha kuturejesha tena mjini katika mazingira ya shule.

Jambo la pili linaloipa hadithi yenyewe mvuto wa kipekee ni jinsi mwandishi alivyolisimulia suala la utunzaji wa mazingira kwa kuwatumia watoto kama wahusika wakuu wa jukumu hili.

Mnene na wazazi wake wanafunga safari kutoka jijini Nairobi kwenda Taveta kumtembelea Ami Kodawa.

Mwandishi anaichelewesha safari hiyo inayojiri katika muhula wa tatu kusudi ili kutudhihirishia udhia unaoandamana na usafiri hasa muda wa Krismasi unapokaribia.

Katika kituo cha mabasi cha Nyamakima ambapo msimulizi na wazazi wake wanakwenda kukata tiketi ya basi, watu waliobanana kama utitiri wanang’ang’ania mabasi machache yanayopatikana kituoni.

Kule Ngonyi, Ami Kodawa anawakaribisha wageni kwa kuwachinjia beberu.

Mnene na binamu yake Dingiria wanachukua pikipiki ya Ami Kodawa na kuanza kuiendesha.

Uchakaramu wa ujana unamfanya Mnene kuiendesha pikipiki kwa kasi kupitia mbuga ya wanyama akitaka kuliwasilia soko la Ngonyi.

Chatu

Ni humu mbugani ambapo pikipiki ambayo kijana huyu anaiendesha kwa mwendo wa kasi inakutana ana kwa ana na chatu.

Kujirusha kutoka juu ya pikipiki kunamfanya Mnene kugongesha goti lake kwenye kichuguu na kuumia.

Maafisa wa Huduma kwa Wanyamapori wakiongozwa na Sengeti ndio wanaombeba Mnene na pikipiki yake kwenye gari lao, wanampeleka hospitalini anakotibiwa goti lake na hatimaye kumrejesha nyumbani kwao.

Kilele cha hadithi hii ni katika shule ya Heresta ambapo shule hiyo inaibuka mshindi katika mchezo wa kuigiza wenye mada ‘Mazingira Mufti’.

Huu ni mchezo uliotungwa na Mnene kwa kuchochewa na ziara yake kwa Ami Kodawa ambapo alishuhudia uharibifu wa Ziwa Jipe.

Lugha tononofu yenye ucheshi imetumiwa kuisuka hadithi hii miongoni mwa mbinu nyingine.