Makala

MAPITIO YA TUNGO: Musaleo! Riwaya inayoumulika uongozi wa kimabavu kitashtiti

April 24th, 2019 2 min read

Jina la utungo: Musaleo!
Mwandishi : K.W Wamitila
Mchapishaji: Vida-Muwa
Mhakiki: Nyariki Nyariki
Kitabu: Riwaya
Kurasa: 102

MUSALEO ni ufupi wa ‘Musa wa Leo’ – lakabu anayopewa kiongozi wa taifa na vibaraka wake.

Majina mengine anayoitwa ni pamoja na Mtukufu Mzee, Mzee, Mwalimu Namba Moja, Mganga, Mleta Mvua, Life President na kadhalika.

Riwaya hii inaukejeli uongozi wa kimabavu katika taifa linalostawi kwa matumizi ya jazanda na tashtiti inayowasha kama upupu.

Zipo simulizi mbili zinazoenda sambamba. Hadithi moja inasimuliwa na Kingunge, mwandishi msifika.

Simulizi ya pili inamzunguka Mugogo Wehu.

Simulizi ya Kingunge ni hadithi ndani ya hadithi. Kwenye simulizi hii, Musaleo anamtaka Profesa kufanya utafiti ili kung’amua asili ya jina ‘Ukolongwe’ ambalo Musaleo aliitwa na babu yake.

‘Ukolongwe’ inaibukia kuwa jazanda ya kiongozi wa enzi ya ukoloni.

Asili yake ni nchi ya Njaamani.

Alipohamia katika nchi ngeni, inasemekana kuwa Ukolongwe alikuwa na umri wa miaka michache sana.

Utafiti wa Profesa unadhihirisha kuwa hakuwa mtoto wa kawaida kimaumbile na kitabia.

Alikuwa mfupi, mwenye kichwa kikubwa ajabu na nywele zisizoiva. Alikuwa na kiburi kingi kiasi cha kuthubutu kuwajibiza wazee hadharani hata katika ugeni wake.

Wazee walimchukulia tu na kumpa ardhi ya kujenga nyumba katika mji wa Masa.

Hivi ndivyo Ukolongwe na jamaa zake walivyoishia kustawisha istiimari.

Wenyeji wanaishia kusukumwa kwenye ardhi kame na kaufu. Kilele cha uongozi wa Ukolongwe kinakuwa kupandikiza utamaduni wake juu ya utamaduni wa wenyeji kwa kuamrisha kuchongwa kwa ‘mbuyu wa kijiji’ kisha juu yake akasimika bendera ya ufalme wake.

Ukombozi

Huu ukawa mwanzo wa harakati za wenyeji kujikomboa. Ukolongwe haondoki kabla ya kujipenyeza katika bongo za wenyeji.

Hadithi ya Mugogo Wehu, ambayo kufikia mwisho wa riwaya inaoana na kisa cha Kingunge, inasimulia kuhusu ukoloni mamboleo.

Mugogo Wehu anapambana na mfumo wa kidikteta ambao kiongozi wake ni ‘Mzee’ anayesimuliwa katika hadithi ya Kingunge.

Uongozi wa ‘Mzee’ umejaa dhuluma za kila aina zikiwamo mauaji ya ‘watoto’ kwa kisingizio cha kukabiliana na uovu.

Upelelezi wa mauaji haya ndio unaomwingiza Mugogo Wehu Matatani.

Anatiliwa sumu kwenye maji ya kunywa na Anima, mpenziwe, kutekwa nyara.

Mugogo Wehu yuko mahututi mawazo yake yanapopelekwa katika nchi nyingine ambapo anakutana na waliouawa chini ya uongozi wa ‘Mzee’.

Miongoni mwa watu hao ni yule Profesa aliyemfichulia siri ya jina Ukolongwe, Ngwena aliyekuwa mshauri mkuu wa Mzee, na Kasuku – mmoja wa viongozi shupavu wa kundi la ‘Vijana wa Mzee’.