Makala

MAPITIO YA TUNGO: 'Naomba Unisamehe' ni novela inayotaka wazazi kukubali radhi za wana wao

September 18th, 2019 2 min read

Mwandishi: Ambaka Vusala

Mchapishaji: Kenya Literature Bureau

Mhakiki: Wanderi Kamau

Kitabu: Novela

Jina la Utungo: Naomba Unisamehe

Kurasa: 38

MSINGI wa maadili mema huwa ni malezi yafaayo.

Malezi huakisi methali isemayo kuwa ‘mti uwahi ungali mdogo.’ Hilo ndilo suala kuu analolizamia mwandishi Ambaka Vusala, kwenye novela ‘Naomba Msamaha’.

Ni hadithi inayowahusu wavulana wawili; Musalia na Otiende.

Musalia anasawiriwa kuwa mwenye maadili mema, ikilinganishwa na mwenzake, Otiende.

Hadithi inapoanza, Musalia anachukua gari lake la kujitengenezea na kuanza kuliendesha, ambako anakutana na rafikiye Otiende akiwa anawachunga ng’ombe wao.

Baada ya kumshawishi, Otiende anaacha kuwachunga ng’ombe na kuanza kuliendesha gari hilo. Kwa hivyo, wanaondoka malishoni na kuvamia shamba la mahindi lililokuwa karibu.

Haya yote yakifanyika, Otiende hakuwa karibu wala kufahamu. Kwa bahati nzuri, Bi Mmboga, aliyekuwa akipita karibu na shamba hilo anawaona ng’ombe hao, anawaondoa shambani. Baada ya muda, Otiende na Musalia wanarejea, ila wanakuta kwamba mambo si mazuri.

Wanajaribu kujificha, ili kutoadhibiwa na Bi Mmboga. Hata hivyo, Otiende anaibukia kuwa katika njiapanda; atoroke ama asitoroke. Mawazo hayo yanampa usumbufu mwingi.

Anaamua kunyenyekea na kuomba msamaha kwa Bi Mmboga, akikiri kutenda maovu kwa kuwaruhusu ng’ombe wao kuvamia shamba la wenyewe na kuharibu mimea.

Kama mzazi anaelewa na kukubali rai ya mwanawe. Bi Mmboga anamsamehe. Otiende anasikitikia kosa lake, akiahidi kutorudia tena.

Hali ni kinyume kwa Musalia, ambaye anachukua gari lake na kutoroka. Njiani, mkosi haukosi kumwandama kwani anamgonga Mzee Alumasa, mguuni na kumjeruhi. Mzee Alumasa alikuwa akiendesha baiskeli. Kutokana na kasi ya gari hilo, anaanguka na kugaagaa kwa uchungu, ambapo pia anapata jeraha mguuni. Baada ya maumivu yake kupungua, anajikokota na kuendelea na safari yake.

Musalia anajificha baada ya tukio hilo, ila anatokea baada ya Mzee Alumasa, ambaye alikuwa rafikiye babaye kuondoka.

Mzee Alumasa anamkaripia vikali, lakini anamshauri kutorudia makosa hayo. Licha ya hayo, Mzee Alumasa anamfahamisha babaye Musalia kuhusu kisa hicho.

Kinyume na Mzee Alumasa, babaye anamwadhibu vikali, licha ya kuomba msamaha.

Otiende anaibukia kujutia vitendo vyake na kuomba msamaha. Mwandishi anasisitiza umuhimu wa wazazi kukubali radhi za watoto wao, ikiwa wanagundua makosa yao.

 

[email protected]