Makala

MAPITIO YA TUNGO: Ndoto ilivyotumiwa kufanikisha maudhui katika ‘Upepo wa Mvua’

August 28th, 2019 2 min read

Jina la utungo: Upepo wa Mvua

Mwandishi: Jeff Mandila

Mchapishaji: The Jomo Kenyatta Foundation

Mhakiki: Nyariki Nyariki

Kitabu: Tamthilia

Kurasa: 102

KATIKA ndoto ya Kidani, umo uhalisia mchungu.

Umaskini umeyafikisha masomo ya Kidani na dada yake, Waadi, katika hatima ya ghafla. Umaskini huo ndio unaokuwa kichocheo cha ndoto ya Kidani.

Anaota akiwaongoza wanakijiji wa Bondeni kuunyonyoa mbawa uongozi mbaya wa Chifu Mtoro ambao unakipendelea kijiji cha Mlimani kinachoendelea kiuchumi huku wakazi wa Bondeni wakiendelea kupiga kachombe katika bahari pana ya umaskini.

Mambo kadha yanaelekea kuwa kizingiti kwa Kidani katika kuitimiza ndoto yake ya ukombozi. Kwanza, hana elimu ya kutosha ya kumtilia pondo. Tayari yeye na dada yake wamefurushwa shuleni kwa kushindwa kulipa karo. Pili, mama yake hataki mwanawe kujitosa katika siasa kwa sababu kadha.

Mosi, anauhofia usalama wa Kidani kwani hataki yaje kumkumba yaliyomkumba baba yake, Mhina, ambaye pia alikuwa mtetezi wa wanyonge. Pili, mama anaithamini sana elimu ya mwanawe na anajitahidi kwa jino na ukucha kuhakikisha kuwa Kidani amerudi shuleni kujipiga msasa kabla ya kujitosa katika siasa.

Mwisho, mama anahofia kuwa huenda wanaotetewa wakaishia kumsaliti mwanawe na kumwacha kwenye lindi la mashaka.

Sehemu ya kwanza ya tamthilia inatamatikia pale ambapo Kidani amepigwa na kuumizwa na Chifu Mtoro kwa kuupinga uongozi wake.

Papo hapo, Kidani anazindukana kutoka usingizini. Sehemu inayofuata ya tamthilia,inaonyesha hali halisi ya aila ya Kidani na jamii ya Bondeni kwa jumla.

Akina Kidani hawana chochote cha kujivunia.

Hawana hata kamba ya kumfungia mbuzi ambaye anarandaranda na kuivamia mimea ya Timbakwiri.

Juhudi za Kidani za kutaka kuikomboa jamii yake sasa zinajidhihirisha katika uhalisia wake. Jambo hili linajidhihirisha kupitia ujumbe wake wenye uzinduo kwa jamii.

Ujumbe huu ndio hatimaye Timbakwiri, Oriang na Msa – wawakilishi wa Bondeni – wanaufikisha kwa Chifu Mtoro.

Chifu Mtoro anaahidi kuufanyia mapinduzi uongozi wake.

Ndoto, mbinu rejeshi na majazi ni miongoni mwa mbinu ambazo Mandila amezitumia kwa ufundi mkubwa katika kuyasuka maudhui yake.

Hadithi inaanza kwa ndoto ya Kidani ya kukikomboa kijiji cha Bondeni.

Ndani ya ndoto mna mbinu rejeshi inayoufanya mwisho wa tamthilia kuwa mwanzo wake. Mwandishi amezitumia mbinu hizi mbili kwa ufundi wa hali ya juu.