Makala

MAPITIO YA TUNGO: Pepo za Mizimu; Novela faridi kuhusu mizimu na nafasi yake katika jamii

November 27th, 2019 2 min read

Mwandishi: Ali Attas

Mchapishaji: Moran Publishers

Mhakiki: Wanderi Kamau

Kitabu: Novela

Jina la Utungo: Pepo za Mizimu

Kurasa: 88

UWEPO wa mizimu ulikuwa baadhi ya itikadi ambazo zilihimili maisha ya kila siku ja jamii za kikale za Kiafrika.

Katika jamii hizo, mizimu ilionekana kama aina ya miiko ambayo kwa namna moja, ilitekeleza majukumu muhimu kama kuonya, kutahadharisha, kuelimisha, kulainisha kati ya majukumu mengine muhimu.

Aghalabu hadithi nyingi ambazo zilitambwa katika jamii hizo zilijikita katika ‘maajabu’ ya mizimu, kama inavyodhihirika kwenye novela ‘Pepo za Mizimu’ iliyoandikwa na Ali Attas.

Ni kitabu cha kipekee ambacho kinajikita katika maajabu na shani za mizimu anazokutana nazo Kijana Juma, kwenye safari ya kufika katika makao dhahania ya Mizimu.

Hadithi inaanza pale Mzee Manyonga, babake Juma anapokaribia kufariki. Katika maisha yake, Mzee Manyonga aliogopwa na wanakijiji wa kijiji cha Kigano, kwani waliamini kwamba “alifuga” viumbe ambao hawakuwa na maumbile ya kibinadamu.

Lakini kinyume na dhana za wanakijiji, simulizi za Mzee Manyonga ni tofauti sana, hasa anapomshauri Juma kuhusu namna angetumia viumbe hao kujifaa na kuisaidia jamiii yake.

Kwanza, Mzee Manyonga alikuwa akimfuga bundi, kiumbe ambaye hadi sasa anaogopwa na wengi. Pili, alikuwa na kofia maalum aliyoiitwa “Shumburere” ambayo ilikuwa na ‘siri’ nyingi. Miongoni mwa siri hizo ni mbinu ambazo Juma angetumia kujiepushia mazingaombwe, ikizingatiwa kuwa kwa upana, maisha ya jamii za kizamani mambo kama uganga yalikuwa sehemu ya tamaduni zao.

Baada ya Mzee Manyonga kufariki, mkewe anaugua sana, huku familia yake ikikumbwa na hali ya ufukara. Juma na mamake wanakosa chakula, kiasi cha kutegemea uji pekee.

Hata hivyo, Juma anatumia busara aliyoachiwa na babake kuokoa hali mbaya ya mamake. Kwanza, anafika katika mti mmoja aina ya mbuyu ambapo anatumia ‘siri’ ya “Shumburere” kutafuta mabuyu ambayo wanatumia kama chakula. Hilo linawaepushia makali ya njaa.

Lakini kabla ya kufanikiwa kupata mabuyu kwa mamake, anadanganywa na bweha mkorofi kwamba matunda aliyobeba kupeleka nyumbani hayakuwa mabuyu.

Licha ya hayo, anafanikiwa kujiepusha na hadaa za bweha huyo kwa mara ya pili.

Miujiza mingine tunayoshuhudia ni wanyama wakibadili sura na maumbile yao, hasa anapoanza safari ya kuelekea katika makao ya Mizimu.

Pia, kwa uwezo ambao amepewa na marehemu babake, anaingiliana na wanyama hatari kama nyoka ambao hawamdhuru kwa vyovyote vile.

Kilicho wazi katika kitabu hiki ni kwamba mizimu ilikuwa mojawapo ya tamaduni ya jamii za Kiafrika, ila imeendelea kufifia kadri usasa unavyozidi kutaasisika. Mwandishi pia anaumbua dhana kwamba haikuwa na manufaa yoyote kwa jamii.

Changamoto yake kuu ni kwamba licha ya usasa huo, tamaduni hizo zitabaki kama kitambulisho kikuu cha asili yetu kama Waafrika.

 

[email protected]