Makala

MAPITIO YA TUNGO: 'Usiku wa Mashaka' ni riwaya inayotambua juhudi dhati za polisi

July 31st, 2019 2 min read

Mwandishi: Ngulamu Mwaviro

Mchapishaji: One PLANET

Mhakiki: Nyariki Nyariki

Kitabu: Riwaya

Kurasa: 124

NGULAMU Mwaviro anatuchorea taswira chanya ya vyombo vya dola ambavyo aghalabu hulimbikiziwa lawama kwa kuzembea kazini.

Kupitia Sajini Rosalia, Mwaviro anatudhihirishia kuwa wangalipo maafisa katika idara ya polisi ambao wamejitolea kufa kupona kazini licha ya changamoto chungu nzima zinazowazunguka.

Kwa hivyo, haihalisi kuilaumu idara nzima ya polisi.

Sajini Rosalia, kwa ushirikiano na maafisa wengine, anapata ufanisi mkubwa katika kukomesha matukio mawili makuu ya uhalifu katika nchi yake.

Aila ya Bwana Kitando inavamiwa na majambazi matatu yanayoilazimu kupakia vitu vya nyumba kwenye lori wanaloliegesha nje ya nyumba yao iliyo katika mtaa wa Halua.

Majambazi yenyewe yanamshurutisha Bi Kitando kuwasadikisha majirani kuwa walikuwa wameamua kuhama kwa dharura usiku huo kwa kuwa walikuwa wamepata jumba kubwa katika mtaa wa Ngede.

Baada ya kuwaaga majirani, shehena inapakiwa kwenye lori linalong’oa nanga kuelekea kusikojulikana.

Huu unakuwa usiku wenye mashaka tipitipi kwa familia ya Kitando na mpwa wao, Kangwana, ambaye ni mara yake ya kwanza kukumbana na tukio kama lile. Bi Kitando anabanwa baina ya majambazi wawili mbele ya lori ilhali Bwana Kitando, Mkondo, Pendo na Kangwana wanaingizwa nyuma ya lori baina ya mizigo.

Lori linapitia vijia vya mkato ili kukwepa vizuizi vya polisi. Mvua inakunya bila kupusa. Lori linatelezateleza na kuingia kwenye mtaro.

Bwana Kitando na aila yake wanalazimishwa kulikwamua kutoka mtaroni.

Wanapofika Thika Super Highway, wanakumbana na kizuizi cha polisi. Bi Kitando analazimishwa kuwaambia polisi kuwa yeye ndiye mwenye mizigo na kuwa alikuwa akihamishwa.

Maelezo

Kangwana anafanikiwa kuandika maelezo fulani kwenye karatasi ya katoni na kuitupa nje kupitia upenyu kwenye turubali.

Haya ndiyo maelezo ambayo baadaye yanatumiwa kulisaka gari lile lililohusika katika wizi na utekaji nyara.

Majambazi yale yenye mitambo ya kunasa mawasiliano ya polisi yanafanikiwa kuvikwepa vizuizi vyote vya polisi. Yanaiacha aila ya Kitando kwenye msitu mkubwa na kuondoka na mpwa wao; Kangwana.

Lori linawasili katika shamba la mikonge lililopo Machakos. Shehena inapakuliwa na kuwekwa kwenye bohari kubwa ambalo pia linatumiwa kama malazi.

Mle msituni walimoachwa, Mkondo anashikwa na kichomi.

Kikohozi chake kikavu kinawasaliti zaidi kwani wanajipata kwenye himaya mpya ya Bwana Morgan; kaburu anayejihusisha katika biashara haramu ya ukuzaji wa bangi msituni na uuzaji wa viungo vya wanyamapori.

Msako wa Sajini Rosalia unafanikiwa kumnasa mkuzaji wa bangi na wale wanyang’anyi wanaoiteka aila ya Bwana Kitando.