Makala

MAPITIO YA TUNGO: Vipawa Vya Hasina; Masimulizi yanayoipigia chapuo elimu ya msichana

September 11th, 2019 2 min read

Jina la utungo: Vipawa vya Hasina

Mwandishi: Said A. Mohamed

Mchapishaji: Oxford

Mhakiki: Nyariki E. Nyariki

Kitabu: Hadithi ya watoto

Kurasa: 46

KATIKA masimulizi haya, Said Mohamed ameonyesha kwamba inawezekana wazazi wachochole kujinyima ili watoto wao; hasa wale wa kike, wapate elimu na kujiandalia mustakabali.

Bwana Badi na mkewe wanajisabilia nafsi ili kumpa binti yao elimu.

Hadithi inaanzia shambani katika kijiji cha Kidongo ambapo Hasina anaota ndoto ya kukinai elimu kuwa mtu mkubwa ili aliwasilie jiji atagusane na watu wake na hata kuishi maisha ya kifahari kama wao.

Ndoto ya Hazina ya kufika jijini inatimia pale ambapo wazazi wake wanaiuza mifugo yao yote na kuguria jijini ambapo wanakwenda kuishi kwenye kibanda cha Marehemu Kasimu ambaye alikuwa mjombawe Hasina.

Ijapokuwa Mzee Badi anafanya kazi ya kijungu meko ya kuchimba na kuosha mitaro anajisabilia nafsi na kumpeleka binti yake katika shule bora na ya kifahari ili naye apate kukinai kiu yake ya masomo.

Katika shule ya upili ya Weupeni, Hasina anakumbana na changamoto kadhaa kubwa zaidi ikiwa kubezwa na wanafunzi wengine wanaotoka katika aila za kitajiri na wanaomwona kuwa hafai kuwa katika shule hiyo ya ‘vigogo’.

Wanafunzi hao wanaponunuliwa karatasi za shashi wanazozitumia msalani, Hasina anatumia vipande vya magazeti kwa kuwa wazazi hawana uwezo wa kumtimizia starehe ile. Hasina hana pesa za masrufu wala nguo za kifahari kama walizo nazo wasichana hao.

Kwa kutia bidii masomoni na kuuzingatia ushauri wa Bi Zenu, mkuu wa shule, Hasina anaishia kushikilia nafasi ya kwanza masomoni.

Weledi huo katika masomo na rundo la vipawa alivyo navyo kikiwamo kile cha kuigiza vinawafanya wanafunzi na walimu waliombeza kuanza kumpenda na kumheshimu tena.

Hulka nyingine inayojidhihirisha kwa Hasina ni ile ya kuwaambaa marafiki ambao anahisi wangemponza.

Sikuukuu, rafiki yake, ambaye anamtetea dhidi ya uchokozi wa wasichana wengine, anapojaribu kumwingiza katika mtego wa kuchuuza mili yao kama njia moja ya kujipatia pesa za masrufu, Hasina anaona hatari na kumwambaa.

Hadithi inakamilika kwa furaha na tanzia. Furaha yenyewe inatokea pale ambapo Hasina anaupasi mtihani wake wa kidato cha nne bila kiasi kwa kuzoa A nyingi.

Tanzia inajiri Sikuukuu anapougua na hatimaye kuaga dunia kwa kuambukizwa ndwele ya UKIMWI.

Lugha iliyotomelewa tamathali mbalimbali za usemi ni mojawapo ya mambo yanayoipa hadithi mnato wa pekee.