Makala

MAPITIO YA TUNGO: Miaka 52 Jela; Tawasifu aali kuhusu jela na dhiki zake enzi za ukoloni

June 26th, 2019 2 min read

Mwandishi: Michael Karanja Ngugi

Mchapishaji: Heinemann Kenya

Mhakiki: Wanderi Kamau

Kitabu: Tawasifu

Jina la Utungo: Miaka 52 Jela

Kurasa: 123

SAFARI ya Mzee Michael Karanja Ngugi ni ya kuogofya.

Ni simulizi ambayo kwa namna moja, inamwacha msomaji na mawazo mengi kuhusu vile anajipata gerezani kwa karibu robo tatu ya uhai wake.

Amesimulia maisha yake kwenye tawasifu ‘Miaka 52 Jela.’ Alizaliwa mnamo 1919 katika Kaunti ya Murang’a, wakati huo ikijulikana kama wilaya.

Huu ulikuwa ni wakati ambapo Waingereza walikuwa wameanza kuingia nchini na kubuni makanisa katika sehemu mbalimbali nchini—kupitia Wamishenari.

Kama watoto wengine wa Kiafrika, Mzee Karanja anazaliwa katika mazingira magumu sana; ya umaskini na mahangaiko.

Hilo lilimfanya kuajiriwa kama mchungaji katika makazi ya bwanyenye mmoja katika eneo la Gilgil.

Hata hivyo, makali ya njaa yanamfanya kuanza kujiingiza katika wizi wa vyakula katika mashamba ya watu.

Anaungana na wavulana wenzake, ambapo mtindo huo unaendelea hadi pale anapokamatwa wa wanakijiji anaowaibia na kuchapwa.

Nyuma kidogo, mojawapo ya sababu ambazo zinamfanya kutoroka kwao Murang’a ni vifo tata vya wazazi wake, anaoamini kwamba walirogwa.

Babake alifariki akiwa kitoto kidogo. Mamake naye anaachwa kuwalea katika mazingira magumu sana, ambapo kwa wakati mwingine alishindwa kuwakimu.

Masaibu zaidi yanaendelea kuwakumba, baada ya mamake pia kufariki katika hali tatanishi—anarogwa pia!

Masaibu yanapozidi, anatoka Gilgil na kuhamia jijini Nairobi, anakoajiriwa katika mojawapo ya maduka ya Wahindi.

Anafungwa jela kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 17 pekee.

Baadaye, anatoka, baada ya kuhurumiwa kutokana na umri wake mdogo.

Anarudi Murang’a kwa kutumia lori moja, lakini hakuacha hulka ya wizi. Humo, anaendelea kuiba mazao katika mashamba ya watu, hali inayomfanya kukamatwa tena na kupigwa sana. Mara hii, ananusurika kuchomwa.

Anashtakiwa kwa chifu, anayemwamuru awe akiripoti katika afisi yake kila baada ya wiki moja. Hali inapomzidia, anarudi Nairobi na kuajiriwa tena.

Anajiunga na makundi ya wahalifu ambapo wanashiriki katika vitendo vya wizi katika maduka mbalimbali ya Waafrika maarufu na Wahindi.

Wanakamatwa katika kisa kimoja cha wizi, ambapo wanahukumiwa kifungo cha maisha.

 

[email protected]