Mapolo wasaka mwizi wa asali

Mapolo wasaka mwizi wa asali

Na JOHN MUSYOKI
BANANA, KIAMBU

JAMAA mmoja aliyedaiwa kuchovya asali kwa mama pima na kutoroka anasakwa na mapolo waliodai aliramba asali yao.

Inasemekana jamaa anatoka mtaa jirani na ni juzi tu alianza kujivinjari kwa mama pima. Kulingana na mdokezi, alimrushia chambo na mama huyo akaingia boksi.

“Alianza kustarehe na mama pima chumbani jambo lililowakasirisha mapolo waliokuwa na uhusiano wa karibu na mama pima,” alisema mdokezi

Siku ya kioja baada ya mapolo kupata habari kwamba mama pima alikuwa na dume mwingine, walilalamika na kuapa kumsaka jamaa kumkomesha kwa kuwanyang’anya mpenzi wao.

Mapolo walisikika wakipiga kelele kilabuni huku wengine wakidai mama pima alikuwa mtu wao kwa siku nyingi. “Ni nani huyo alikuja hapa na kuchukua usukani. Haiwezekani mtu kuwa na dharau kiasi cha kuvamia kijiji chetu na kutupokonya asali. Nikimpata aliyekuwa akichovya asali yangu nitamnyorosha,” jamaa mmoja alisikika akiwaambia wenzake.

Naye mwenzake alisikika akilalamika pia. “Ni mimi mume rasmi wa mama pima na tulikuwa tumepanga kuoana kabla ya jamaa kuharibu mambo. Nitamsaka huyo mwizi wa mapenzi na nikimpata atakiona cha mtema kuni,” jamaa alisikika akimwambia wenzake.

Inasemekana baada ya siku chache, mama pima aliwatumia waliokuwa wakilalamika ujumbe na kuwasihi wamkome kwa sababu tayari alikuwa ameamua kuolewa na jamaa aliyehusishwa naye.

Mapolo walituliza boli baada ya kitumbua chao kuingia mchanga. Hata hivyo haikujulikana iwapo mama pima aliolewa na jamaa licha ya fununu kuenea kote mtaani kwamba alikuwa akimtamani kwa sababu ana mihela tele kuliko mapolo wa mtaani waliokuwa wakimmezea mate.

You can share this post!

Mbunge ashauri KWS kuajiri wawindaji haramu, eti wana ujuzi!

NGILA: Mazuri ya teknolojia kwa ajira yanazidi mabaya yake

adminleo