Makala

MAPOZI: Bensoul

July 16th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

ALIKUWA mwanamuziki wa kwanza kusajiliwa na Sol Generation, lebo inayomilikiwa na bendi ya Sauti Sol.

Jina lake ni Benson Mutua al-maarufu Bensoul Muziki, mwanamuziki, mwandishi wa nyimbo, produsa na mcheza ala za muziki. Yeye ni mmoja kati ya wasanii sita walioshirikishwa kwenye kibao Extravaganza, chao Sauti Sol.

Lakini licha ya kwamba wimbo huo ulichangia pakubwa kumpa mfichuo na umaarufu, Bensoul anajivunia pia kazi zake kama mwanamuziki solo.

Anatambulikwa kwa nyimbo kama vile Lucy, Not Ready, Gloomy Morning, I Only Wanna Give It To You, Rastafari, Ningependa Nikuchukie na What We Lost miongoni mwa zingine.

Benson Mutua maarufu ‘Bensoul Muziki’ ni mwanamuziki wa kwanza kusajiliwa na Sol Generation, lebo inayomilikiwa na bendi ya Sauti Sol. Picha/ Maktaba

Kinachomtofautisha na wasanii wengine ni ustadi wake wa kucheza ala mbalimbali ikiwa ni pamoja na ngoma, fidla na gitaa.

Aidha, Bensoul anafahamika kwa ushupavu wake katika uandishi wa nyimbo. Anajivuinia kuandikia nyimbo baadhi ya majina makuu kama vile Sauti Sol, Kidum, AliKiba, Nyashinski, Benpol, H_Art the Band na Mercy Masika, miongoni mwa wengine.

Ni ustadi huu ambao umemfanya kutambuliwa na wasanii wengine wa haiba ya juu. Kwa mfano wakati mmoja, mmojawapo wa wanachama wa Sauti Sol – Bien-Aime, alimtaja kama mwandishi shupavu wa muziki.

Pia, mwaka 2018 aliungana jukwaani na mwanamuziki Chronixx kutoka Jamaica katika mojawapo ya shoo zake nchini, huku msanii huyu akimtambua kama mmojawapo wa wanamuziki shupavu wa kutazamiwa siku zijazo.

Ni suala hili ambalo limemfanya kuteuliwa katika tuzo mbalimbali. Mwaka wa 2017 aliteuliwa kama mwanamuziki bora wa mwaka wa mdundo wa soul katika tuzo za Café Ngoma Awards.

Aidha, mwaka jana, kibao Masheesha, alichoimba kwa ushirikiano na H_ART The Band kiliteuliwa katika kitengo cha kolabo bora ya mwaka kwenye tuzo za Pulse Music Video Awards (PMVA).

Huenda hii ndio mojawapo ya sababu ambazo zimemfanya kuwa kivutio hata miongoni mwa wanamuziki wenzake.

Bensoul alitambua kipaji chake akiwa angali mdogo, wakati huo akiishi mjini Embu pamoja na familia yake, huku akitumia jukwaa la kanisa kujikuza kimuziki.

Ajifunza kucheza ala

Akiwa pale alikuwa akichukua ala tofauti za muziki na kujifunza kuzicheza.

Baada ya kukamilisha masomo ya upili alihamia jijini Nairobi ambapo alikutana na wanachama wa bendi ya H_Art The Band na kuwa marafiki.

Alijiunga na chuo cha Sauti Academy na baadaye akasajiliwa na lebo ya Sol Generation kabla ya kuangusha kibao Lucy.

Baadaye alitunga vibao vingine ikiwa ni pamoja na Ntala Nawe, Not Ready, Don’t Question My Love na Ningependa Nikuchukie, wimbo uliopokelewa vyema hasa katika mtandao wa Soundcloud. Aliandika kibao hiki kuzungumzia jinsi mama yao alivyotaabika kumlea pamoja na nduguze bila usaidizi wowote hasa kutoka kwa baba mzazi.

“Nakumbuka kuna nyakati ambapo nyumba yetu ingefungwa kwa sababu ya kutolipa kodi. Wakati mmoja dada yangu alilazimika kuacha shule ili nipate fursa ya kuendelea na masomo. Kutokana na hayo, tulihangaika sana ambapo ujumbe huu ulinuia kumfikia babangu,” alisema wakati mmoja katika mahojiano.

Kwa sasa ingawa bado hajakita mizizi vilivyo katika fani ya muziki, ni dhahiri kwamba Bensoul anazidi kujiundia jina kama mojawapo ya majina yenye ushawishi katika fani hii. Lililosalia ni yeye kuhakikisha kwamba anatimiza utabiri wa wengi wanaotambua uwezo wake kimuziki.