Makala

MAPOZI: Cedo

June 25th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

JINA lake linapotajwa, basi huandamana na orodha ya baadhi ya majina makuu katika muziki nchini vilevile vibao maarufu.

Jina lake ni Cedric Kadenyi lakini miongoni mwa mashabiki anafahamika kama Cedo, mwelekezi na produsa wa muziki wa kampuni ya Pacho Group Limited, aliyeamua kuacha taaluma yake kama wakili na kujitosa katika burudani.

Anafahamika hasa kama produsa, mhandisi, mcheza piano na hata mwandishi wa nyimbo huku akisifika kwa kutoa huduma zake kwa baadhi ya wanamuziki wanaotambulika nchini na mbali.

Baadhi ya vigogo aliofanya kazi nao ni Sauti Sol, Nyota Ndogo, Hart the Band, Nyashinski, Dela, King Kaka, Kristoff, Everlast, Naiboi, Redsan, Amos and Josh, Frasha na Avril miongoni mwa wengine wengi.

Nje ya Kenya amefanya kazi na wasanii kama vile Chameleon kutoka Uganda, Vanessa Mdee na Rich Mavoko kutoka Tanzania miongoni mwa wengine.

Heshima na utambuzi wake unatokana na baadhi ya kazi maarufu ambazo amezishughulikia. Baadhi ya nyimbo ambazo amerekodi ni pamoja na Sura yako, Mungu Pekee, Masheesha, Adabu, Gudi Gudi, Problem na Badder than Most, miongoni mwa zingine.

Mbali na muziki, pia huduma zake amezipanua na kuhusisha kitambulisho cha baadhi ya mashirika na kampeni maarufu nchini kama vile SportPesa, Mkopa Solar, Mshwari, Kenya Charity Sweepstake, Tusker Jenga Game, Jubilee Insurance, Niko na Safaricom Live, Safaricom Kenya Live na zingine nyingi.

Aidha, alikuwa produsa kwenye msimu wa nne wa shindano la Coke Studio (Season 4).

Ni ustadi huu ambao umemfanya kutambuliwa sio tu humu nchini bali pia nje ya mipaka ya Kenya. Mwaka wa 2013 na 2014 alitambuliwa kama produsa bora wa mwaka kwenye tuzo za Groove Awards.

Mwaka wa 2015, alishinda tuzo ya produsa bora wa mwaka kwenye tuzo za AFRIMA.

Mojawapo ya mambo ambayo yanamtenganisha na maprodusa wengine nchini ni kwamba mbali na kurekodi muziki, yeye ni mcheza piano hodari, suala linalomwezesha kubuni midundo ya kipekee kila anapokaa chini kurekodi nyimbo.

Uwezo wake wa kufasiri mihemko ya mwandishi na kuwa kibao cha kuwasisimua wengi, aidha, umemfanya kujiundia jina, huku sifa yake ya kukumbatia ubunifu na kufanyia kazi aina tofauti za muziki ikimfanya kuwa kipenzi cha wengi.

Mbali na hayo, utaratibu na utafiti anaofanya kabla ya kurekodi nyimbo, umefanya kazi zake kuwa na kina, vilevile kipawa chake cha kuunda uhusiano wa kipekee na wasanii anaoshughulikia kazi zao, vikimfanya kuwa bingwa katika nyanja hii.

Alijitosa katika masuala ya kurekodi muziki kwa mara ya kwanza kati ya mwaka wa 2007 na 2008 huku hasa akishughulikia nyimbo za injili na hata kufanya kazi na baadhi ya majina makuu katika ulimwengu wa muziki wa injili nchini, ikiwa ni pamoja na Kevoh Yout, Mr. T, Maximum Melodies, Betty Bayo na marehemu Kaberere miongoni mwa wengine.

Mwanzo wa safari

Mwaka wa 2011 alikuwa akishughulikia hafla ya Niko na Safaricom Live, na ni wakati huu kazi yake ilivutia bendi ya Sauti Sol, na hivyo kuadhimisha mwanzo wa safari kama produsa wa mojawapo ya bendi maarufu barani.

Kumbuka kuwa wakati huo alikuwa pia akiwafanyia kazi baadhi ya wanamuziki maarufu ikiwa ni pamoja Size 8, Jimmy Gait, Jaguar, Camp Mulla na P-Unit.

Kama produsa wa bendi ya Sauti Sol, alisafiri nao kila mahali na kuhusika katika kila shughuli ya kurekodi muziki wao, suala lililompa mfichuo nchini na kimataifa.

Hata hivyo, baada ya kufanya kazi na bendi hii kwa muda, miaka miwili iliyopita aliamua kushika hamsini zake kujiundia jina kama produsa huru.

Lakini hilo kamwe halijazima azimio lake la kuzidi kung’aa kwani kuambatana na anavyozidisha kasi, bila shaka ni ishara tosha kwamba kamwe hana nia ya kurudi nyuma.