Makala

MAPOZI: Kendi

May 7th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

ALIJITOSA katika ulingo wa muziki akiwa na umri wa miaka 17 pekee na hata kusajiliwa na kampuni ya Calif Records, ambayo wakati huo ilikuwa mojawapo ya lebo kuu nchini.

Nyakati hizo Kendi aliachia vibao kadha vikiwa ni pamoja na Uko Fresh, wimbo uliovumisha jina lake na kumtambulisha kama mmojawapo wa wasanii wa kike walioheshimika nchini enzi hizo, suala lililomfanya kuwa kipenzi cha wengi.

Lakini hata kabla ya kudumu, muziki wake ulianza kudidimia, ishara iliyojitokeza kwenye wimbo wake Uko Fiti ambao haukufanya vyema na kadhalika hakuwahi kuutumbuiza jukwaani.

Haikuwa muda kabla ya msanii huyu kutoweka kutoka fani ya muziki kwa muda huku fununu zikienea kuhusu chanzo cha ukimya wake.

Wakati huu alipamba vichwa vya baadhi ya vyombo vya habari kutokana na uvumi uliohusisha maisha yake binafsi na kimuziki.

Kwa mfano kulizuka tetesi kuhusu ugomvi kati yake na lebo ya Grandpa Records huku akiamua kujitenga na lebo hiyo.

Kulingana naye, ugomvi huo ulitokana na video waliyorekodi lakini haikuzinduliwa, vile vile video nyingine ambayo alihisi kana kwamba haikusukumwa jinsi alivotarajia.

“Nyakati hizo ilikuwa vigumu sana kushirikiana na msanii wa lebo nyingine au kufanya kazi na kampuni nyingine ya kurekodi nyimbo. Wakati huo nilikuwa nataka kufanya kazi na lebo tofauti katika mradi fulani na uamuzi wangu ukafanya kidogo tukakosa kuelewana, tofauti kabisa na uvumi uliokuwa unaenea,” Kendi alisema katika mahojiano mwaka 2018.

Matatizo haya yalimuathiri nusura aachane na uimbaji isingalikuwa ni msukumo kutoka kwa wanamuziki wengine.

“Wasanii kama vile Avril, Atemi, Sanaipei Tande, Jua Cali, Jaguar na Bahati miongoni mwa wengine walijitokeza kunisaidia kuthibitisha kazi yangu. Isitoshe, Jaguar alinijia binafsi na kunipa moyo,” alisema.

Ni mawimbi yaliyomfanya kukaa mbali na mwangaza wa muziki kwa muda, hadi mwaka jana aliporejea katika fani ya muziki kwa kishindo na mwamko mpya, suala linalodhihirika katika kazi yake murwa.

Kwa mfano aliachia kibao Into You alichoimba kwa ushirikiano na Vinnie Banton.

Kampuni mpya

Vilevile alirudi huku akiwa ameshirikiana na kampuni mpya yenye makao yake nchini Uswidi.

Hapa Kenya kampuni hiyo ilinuiwa kushughulika na kuunda kitambulisho chake kabla ya kuanza kusajili wasanii wengine.

Aidha, tofauti na awali, lebo hii ilitarajiwa kuwa mwamko mpya kwa wasanii wa humu nchini ambapo wangehakikishiwa usalama wa kazi na mapato yao kama mbinu ya kuwapa jukwaa la kung’aa kimuziki.

Aliporejea aliwaahidi mashabiki kwamba tofauti na wasanii wengi nchini Kenya ambao wameshindwa kujinasua kutokana na akili finyu ya kumakinika na Genge, Kapuka na kadhalika, angewaiga wanamuzki kama vile bendi ya Sauti Sol, wanamuziki wa Nigeria na Tanzania ambao wameweza kupanua mawazo yao na kushirikisha mitindo mipya ili kupata mnato wa kimataifa.

Hata hivyo kibao Into You kilichofafanua ujio wake mpya hakikufanya vyema hasa kuambatana ‘views’ kwenye mtandao wa YouTube, suala ambalo hata hivyo alijitetea na kusema kwamba hategemei ‘views’ kubaini umaarufu wa kazi zake na kwamba mwendo wake kurejea katika ulingo wa muziki ni wa asteaste.

Sasa ni mwaka mmoja baada ya kurejea na iwapo kwa kweli ameweza kuafikia utabiri huu, mashabiki ndio wataamua.