Makala

MAPOZI: Maqbul Mohammed

March 12th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

AMETUPAMBIA sebule zetu mara kadha kupitia vipindi vya televisheni ambavyo ni mmoja wa waigizaji.

Kwa wasiomfahamu, anaitwa Maqbul Mohammed, mmojawapo wa waigizaji shupavu nchini.

Hasa sura yake inatambulika kutokana na kushiriki kwake katika kipindi Auntie Boss kama Donovan, mchumbake Eve D’Souza.

Lakini pia mwigizaji huyu anafahamika kwa mchango wake katika vipindi kama vile Makutano Junction, kipindi kilichozinduliwa 2007 ambapo aliigiza kama Karis Mabuki; vingine ni Reflections na Lies that Bind, alipoigiza kama Justine Mareba.

Kando na vipindi, ameshiriki pia katika filamu ikiwa ni pamoja na Behind Closed Doors, Weakness, filamu iliyozinduliwa 2009 ambapo anaigiza kama Nicky na All Girls Together, sinema iliyozinduliwa 2008 na ambapo anaigiza kama Felix.

Ustadi huu umemwezesha kuigiza kando ya vigogo kama vile Eve D’ Souza, Ruth Maingi, Maureen Koech, Justine Mirichii na Florence Nduta, miongoni mwa wengine.

Safari yake katika uigizaji ilianza mwaka wa 1995 wakati huo akiwa shuleni ambapo mwalimu wake alimchagua kuigiza katika mchezo fulani kutokana na tabia yake ya kupiga kelele darasani.

Msanii Maqbul Mohammed. Picha/ Hisani

Hata hivyo, ilimbidi asubiri hadi baada ya kukamilisha shule ya upili ili kufufua kipaji chake.

Hii ilikuwa baada ya kutazama tangazo kwenye gazeti kuhusu mchezo fulani wa kuigiza katika Phoenix Theatre.

Aidha weledi huu umechangiwa na sababu kwamba kipaji hiki kimekolea katika familia yao, hasa ikizingatiwa kuwa dadake Shadya Delgush, pia ni mwigizaji.

Kabla ya kuingia kwenye ulingo wa televisheni, alikuwa ashajiundia kitambulisho kwenye thieta huku akiigiza katika michezo ya kuigiza kama vile Backlash, kazi yake Cajetan Boy, drama iliyoangazia unyanyapaa dhidi ya wanaougua Ukimwi.

Kadhalika alishiriki katika mchezo wa Enemy of the People, ulioundwa wakati ambapo nchi ilikuwa inakumbwa na matatizo ya kisiasa huku akitumbuiza mbele ya hadhira iliyojumuisha watu maarufu kama vile Gavana wa Kaunti ya Kisumu, Anyang’ Nyong’o.

Kuacha alama

Na tokea hapo Maqbul hajawahi kuangalia nyuma ambapo amekuwa akiendelea kukinoa kipaji chake huku akizidi kuacha alama thabiti katika safari yake.

Mara yake ya kwanza kujitosa kwenye televisheni ilikuwa mwaka wa 2003, wakati huo bado akiwa katika umri wa kubalehe, aliposhiriki katika kipindi Reflections kilichokuwa kikipeperushwa na kituo cha televisheni cha KBC.

Hata hivyo nyota yake iling’aa mwaka wa 2006 alipopata fursa ya kuigiza kama Karis katika Makutano Junction.

Ni mng’ao ulioendelea na mwaka wa 2011 alikuwa mmojawapo wa washiriki wakuu katika kipindi cha Lies that Bind. Kipindi hiki kilimwezesha kuteuliwa kama muigizaji bora msaidizi katika tuzo za Kalasha 2013.

Na haikushangaza alipopata fursa ya kuwa mhusika mkuu katika kipindi Auntie Boss.

Mbali na hayo yeye pia ni mtangazaji wa redio katika Capital FM.

Kwa sasa ndoto yake ni kung’aa katika jukwaa la kimataifa na hata kujumuika na Lupita Nyong’o kule Hollywood.