Makala

MAPOZI: Nadia

July 23rd, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

HAJADUMU katika fani ya muziki kwa muda mrefu lakini ushawishi wake unahisiwa katika kila pembe ya burudani nchini.

Jina lake ni Nadia Mukami Mwendo, mwimbaji, mwandishi wa nyimbo na mtumbuizaji ambaye sauti yake ya ninga; vilevile ustadi wake wa utunzi, vimemfanya kuorodheshwa miongoni mwa wasanii wanaovuma nchini Kenya kwa sasa.

Kwa vibao kama Yule Yule, African Lover, Lola na Si Rahisi  wimbo ambao umekuwa ukipokelewa vyema na mashabiki – wachache watapinga kwamba Nadia ameonyesha kila ishara za kuiteka fani hii.

Hasa kibao chake cha hivi punde Radio Love kimekuwa pambio kwa wengi huku kikizidi kutawala mawimbi ya stesheni za redio nchini, kwenye matatu na hata vilabuni.

Ni suala ambalo limempa umaarufu na hata fursa ya kutumbuiza pamoja na baadhi ya majina makuu katika ulingo wa muziki nchini.

Mzaliwa wa jiji la Nairobi, Nadia alisoma katika shule ya msingi ya Kari, kwenye barabara ya Nairobi-Mombasa, kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Mount Laverna School, eneo la Kasarani, jijini Nairobi.

Katika shule ya upili, alifanya vyema kwenye mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne, na baadaye kujiunga na Chuo Kikuu cha Maseno ambapo alisomea masuala ya Fedha.

Safari yake kimuziki ilianza akiwa na umri wa miaka 17 pekee huku akichochewa na babake aliyekuwa shabiki sugu wa muziki wa taarab, vilevile mwanamuziki Ray C kutoka Tanzania.

Mara ya kwanza kwake kurekodi muziki ilikuwa baada ya mfanyakazi mwenzake alikokuwa ameajiriwa katika duka la jumla, kumhimiza kwenda studioni.

Ni ushauri ambao aliufuata na kurekodi kibao, Narudi, wimbo uliozungumzia mpenzi mpotevu.

Hata hivyo, safari yake ya uimbaji ilikatizwa kwa muda alipojiunga na Chuo Kikuu cha Maseno.

Hii haikumaanisha kwamba alikuwa ametupilia mbali ndoto yake ya kujihusisha na burudani, kwani alijiunga na idhaa ya redio ya chuo kikuu hicho kwa jina Equator FM, ambapo alikuwa na kipindi chake kwa jina Saturday Hip-hop Count kilichokuwa kikipeperushwa kila Jumamosi.

Baadaye mwaka huo alirejea katika muziki na mwaka wa 2015 alirekodi Barua Ya Siri, wimbo uliopokelewa vyema na mashabiki wake chuoni kutokana na mtiririko bomba wa mashairi.

Kibao hicho kilifuatiwa na Kesi, kilichorekodiwa na Cedo huku kikipeperushwa katika baadhi ya stesheni za televisheni na redio.

Aidha, kupitia wimbo huo aliweza kujihifadhia nafasi katika majukwaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Blaze By Safaricom (Kisumu), Tamasha za muziki za The Nile Festival na The Luo Festival, kando ya baadhi ya majina makuu katika fani ya muziki nchini.

Nyota yake iling’aa zaidi alipoanza kuhudhuria hafla ya Poetry After Lunch (PAL) inayoandaliwa kila Alhamisi katika ukumbi wa Kenya National Theatre.

Mwanamuziki Nadia. Picha/ Maktaba

Ni jukwaa hili lililomwezesha kupata mfichuo zaidi na hivyo kupata fursa ya kuonekana kwa mara ya kwanza kwenye shoo ya Kipawa Show ambapo alitoana kijasho na wanamuziki wengine na kuibuka mshindi.

Pia, alifika katika fainali za shindano la Jenga Talanta, suala lililozidi kumtambulisha na hata kumfanya kupokea mwaliko wa kutumbuiza kwenye Churchill Show, kando ya wasanii wa haiba ya juu kama vile Suzanne Owiyo.

Mwaka wa 2017 alikutana na David Guoro, ajenti wa kusaka vipaji jijini Nairobi, aliyefurahishwa na kipaji na bidii yake, na hivyo kumsajili kwenye lebo yake ya Hailemind Entertainment.

Licha ya kwamba bado hajakita mizizi ambapo machoni mwa wengi pengine bado limbukeni, ukweli ni kwamba Nadia yuko mbioni kuweka jina lake kwenye ramani ya muziki nchini.