Makala

MAPOZI: Produsa R Kay

March 26th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

KWA zaidi ya mwongo mmoja amejijengea himaya kubwa kama mmojawapo wa maprodusa mahiri sio tu humu nchini bali katika kanda ya Afrika Mashariki.

Miongoni mwa mashabiki anafahamika kama R Kay, lakini jina lake halisi ni Robert Kamanzi.

R Kay. Jina lake halisi ni Robert Kamanzi. Picha/ Hisani

Mojawapo ya sifa zinazomtambulisha ni jitihada zake katika harakati za kubadilisha muziki wa Afrika Mashariki kufikia viwango vya juu, suala ambalo limemfanya kuheshimika kiasi cha kuhusuka pakubwa katika kufanya kazi na wanamuziki wengi wanaotamba nchini na mbali.

Baadhi ya wanamuziki wa haiba ya juu kutoka Afrika Mashariki na mbali ambao amewafanyia kazi ni pamoja na Nameless, Ambassada, Jemimah Thiong’o, Esther Wahome, Bahati, Deux Vultures, Bobby Wine, Blue 3, Kidum, Lady Jay Dee, Ray C, Professor Jay, Massamba, Shanel, Jimmy Gait, marehemu Oliver Mtukudzi, Mercy Masika, Rufftone, Suzanna Owiyo, Prezzo na Sanna miongoni mwa wengine, huku mchango wake katika muziki ukidhihirika kupitia takriban albamu 100 ambazo amehusika katika kuzirekodi.

Mojawapo ya sifa ambazo zimezidi kumuundia jina ni msimamo wake mkali hasa inapowadia wakati wa kurekodi muziki, ambapo mara kwa mara amenukuliwa akisema kwamba hawezi kujihusisha na nyimbo ambazo kiwango cha ubora ni cha chini.

Ustadi wake umedhihirika pia kutokana na mchango wake ambao umefanya baadhi ya wanamuziki kutuzwa.

Kwa mfano, mwaka wa 2008 aliweka jina lake katika vitabu vya kumbukumbu kazi yake Sweet Love, wimbo ulioimbwa na Wahu, ulipopelekea mwanamuziki huyu kuwa Mkenya wa kwanza kutwaa tuzo ya MTV MAMA Awards, tuzo kuu barani Afrika.

Sio hayo tu, kibao Sunshine’, kilichoimbwa na Nameless kwa ushirikiano wa Habida, kilimfanya Nameless kutwaa tuzo ya Msanii Bora wa Mwaka wa kiume katika tuzo hizo hizo, mwaka mmoja baadaye.

Hajahusika tu katika kusaidia wengine kutambulika. Kama produsa, R Kay amepokea tuzo mbalimbali.

Ameshinda tuzo humu nchini, Afrika Mashariki na hata mbali ikiwa ni pamoja na Kisima Awards, CHAT Awards hapa Kenya, Channel O Awards (Afrika Kusini), Kilimanjaro Awards za Tanzania, PAM Awards za Uganda, na MTV MAMA Awards, zinazoandaliwa kuwatuza wasanii na washikadau wa burudani barani.

Na katika harakati hizo amezidi kujizolea heshima.

Mwaka wa 2015 alisemekana kupokea donge nono zaidi la kipato kutoka kwa chama cha ukusanyaji hakimiliki ya wanamuziki nchini -MCSK kwa upande wa majukwaa ya kieletroniki, huku pesa hizo zikitokana na mchango wake katika baadhi ya kazi za wanamuziki nchini ikiwa ni pamoja na Nameless, Esther Wahome, Mbuvi, Sarah Kiarie na Eunice Njeri miongoni mwa wengine.

Ushawishi wadhihirika

Ushawishi wake katika sekta hii ulidhihirika hata zaidi kati ya mwaka wa 2003 na 2004, Benki ya Dunia ilipomhusisha pakubwa katika utafiti kuhusu biashara ya muziki nchini.

Penzi lake kwa muziki lilianza akiwa mchanga huku akipata msukumo kutoka kwa babake ambaye alikuwa msanii.

Alihamia humu nchini mwaka wa 1998 kutoka Burundi.

Mwaka wa 1999 alipata ajira katika studio ya Nextlevel Productions ambapo alijifunza kazi yake.

Mwaka wa 2000, aliangusha albamu yake Solutions. Tokea hapo R Kay amefanya kazi na baadhi ya studio kuu humu nchini ikiwa ni pamoja na Homeboyz, Ketebul na Soundmind.

Mbali na kuwa produsa, yeye pia ni mtunzi wa nyimbo, muigizaji, muimbaji na mwelekezi, fani ambazo pia zimemwezesha kujitosa katika ujasiriamali katika masuala ya burudani.