Makala

MAPOZI: Young Wallace

June 18th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

PINDI majina ya baadhi ya waelekezaji wa video matata nchini Kenya yanapotajwa, bila shaka lake huwepo.

Anafahamika miongoni mwa mashabiki kama Young Wallace, Afisa Mkuu Mtendaji wa Convex Media na mmojawapo ya waelekezaji maarufu wa video hapa nchini, huku baadhi ya kazi zake zikiendelea kung’aa karibu na mbali.

Baadhi ya video ambazo ameelekeza ni pamoja na Barua, Tam Tam, Dawa ya Moto, Take it Slow, Kingston Girl, No More, Kamua Leo, Story Yangu, Sijafika, Mpango Wa Kando, One Way, Mungu Yupo na Marungu miongoni mwa zingine.

Na katika harakati hizo ametangamana na baadhi ya vigogo katika ulimwengu wa muziki nchini ikiwa ni pamoja na Bahati, Willy Paul, Size 8, Sauti Sol, Wyre, Kidis, DNA, Wyre, Ameleena, Dennoh, Gloria Muliro, Kambua, Ringtone na Jimmy Gait kwa kutaja tu wachache.

Lakini Young Wallace hajang’aa katika uelekezaji wa video za muziki pekee kwani amepanua huduma zake na kujumuisha matangazo ya kibiashara, vipindi na hata filamu fupi.

Kinachomtenganisha na wenzake nchini ambao huenda vipaji vyao vinatokana na mafunzo pekee, ni ujuzi wake wa kipekee unaochochewa na kiu kiliomsukuma kujifunza kazi hii kupitia mtandao.

Vilevile, ustadi wake unatokana na wepesi wake kimawazo ambao umemwezesha kushughulikia nyimbo za midundo tofauti, vile vile nyimbo za kilimwengu na hata za injili.

Unyenyekevu

Aidha, unyenyekevu wake umekuwa siri ya ufanisi wake ambapo inasemekana kwamba wakati mmoja alimfanyia kazi mwelekezi mmoja nchini bila malipo, katika harakati za kupiga msasa ujuzi wake.

Penzi lake katika taaluma hii lilianza kutokana na kiu ya kusaka kipato.

Wazazi wake waliacha kazi na kuhamia katika maeneo ya mashambani, wakati huo akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia (JKUAT), ambapo pia alikuwa rapa chipukizi.

Lakini baada ya kuimba na kurekodi ngoma yake ya kwanza, hakuwa na senti za kumlipa mwelekezi wa video.

Baada ya jitihada zake za kutafuta pesa za shughuli hii kugonga mwamba, ilimbidi kutumia pesa alizokuwa amepewa na mamake kwa minajili ya kulipa karo kurekodi video, suala lililomlazimu kuacha chuo akiwa katika mwaka wake wa pili kutokana na ukosefu wa karo.

Hakuwa na pesa za kurekodi video yake, na hivyo alilazimika kufanya kazi katika ‘cyber café’ kwa miezi minne huku akijifunza kuhusu masuala ya kompyuta.

Young Wallace. Picha/ Maktaba

Aliamua kufanya utafiti mwenyewe mtandaoni, shughuli iliyomchukua wiki moja na baadaye aliweza kujihariria video hiyo katika studio moja eneo la River Road.

Cha kushangaza ni kwamba baada ya video hiyo kupeperushwa kwenye vituo vya televisheni, kazi yake ilipokelewa vyema na mashabiki.

Wasimamizi wa studio iliyohusika walifurahishwa sana na mapokezi haya hasa ikizingatiwa kwamba awali, kazi zao hazikuwa zimewahi kuchezwa hewani. Hii ilimpa heshima na kumfanya kupewa fursa ya kushughulikia video mle.

Ni hapa alimwendea mwelekezi J Blessing aliyekubali kumfanya msaidizi wake, baadaye akafanya kazi na kampuni ya LB Films kabla ya kuzindua kampuni yake ya Convex Media.

Lakini ufanisi huu haumaanishi kwamba ameweza kujificha kutokana na utata unaoandama wengi kwenye fani ya burudani. Wakati mmoja kuliibuka tetesi kwamba alikuwa ameshindwa kukamilisha kazi za baadhi ya wanamuziki hata baada ya kulipwa.

Lakini licha ya utata huo, amezidi kuwa thabiti katika harakazi zake za kujiundia jina katika fani hii na hivyo kustahili heshima kama mmoja wa waelekezaji video za muziki wanaoenziwa hapa Kenya.