Habari MsetoMakala

Mapuuza ya sheria huleta ufukara, aonya Maraga

March 26th, 2018 2 min read

Na BENSON MATHEKA

JAJI Mkuu (CJ) David Maraga amesema kwamba kupuuzwa kwa utawala wa sheria na ufisadi barani Afrika kumechangia umaskini na kulemaza maendeleo.

Kwenye hotuba yake katika kongamano kuhusu maendeleo barani Afrika lililoandaliwa katika Chuo Kikuu cha Harvard, Amerika, Bw Maraga alisema ni vigumu kutenganisha utawala wa sheria na maendeleo ya dhati.

“Utawala wa sheria na maendeleo vimeunganishwa na vinatiliana nguvu. Utawala wa sheria unatoa mazingira bora ya kushamiri kwa vitendo vyote vya binadamu na ni nguzo ambayo ustawi hujengwa,” alisema Bw Maraga.

“Hata hivyo, katika nyanja ya maendeleo Afrika, haki na utawala wa sheria havichukuliwi kwa umakinifu unaofaa,” aliongeza Bw Maraga.

Alisema kwamba ripoti kadhaa za Umoja wa Mataifa zimetambua kuwa utawala wa sheria na maendeleo haviwezi kutenganishwa.

Bw Maraga alisema kwamba kuimarishwa kwa utawala wa sheria katika viwango vya kitaifa na kimataifa ni muhimu kwa ukuaji na udumishaji wa uchumi, kupiga vita umaskini na njaa.

“Imetambuliwa kuwa utawala wa sheria huleta haki za binadamu ikiwemo haki ya maendeleo zote ambazo huwa zinaimarisha utawala wa kisheria,” alisema.

Alisema utawala wa sheria ni nguzo ya demokrasia. “Umehusishwa na upunguzaji wa mamlaka na nguvu za serikali, uhuru wa mahakama na usawa mbele ya sheria, kulinda haki za kimsingi ziwe za kijamii, kisiasa, kiuchumi, kitamaduni na haki ya mali,” alieleza.

Bw Maraga aliyealikwa kutoa hotuba kuu kwenye kongamano hilo alisema utawala wa sheria unahakikisha kwamba haki za binadamu zinapatiwa uhai kama njia moja ya kupiga vita ubaguzi, kutengwa kwa maeneo na jamii ambazo ni chanzo cha umasikini.

Alisema kwa kuelewa vibaya maana ya utawala wa sheria, sheria hutumiwa kukandamiza wananchi. Bw Maraga alisema Kenya imepiga hatua kubwa chini ya katiba mpya iliyopitishwa 2010 ambayo alisema ilisisitiza utawala wa sheria na jukumu lake katika maendeleo.

Alisema mahakama barani Afrika zinafaa kusaidia bara kufikia utawa bora na kutekeleza haki za kiuchumi na kijami.

“Mahakama ni asasi zinazotoa mchango muhimu katika utawala na hili ndilo jukumu ambazo zinafaa kutekeleza kulingana na sheria. Nchini Kenya, ugatuzi, fedha za umma, masuala ya jinsia zina jukumu muhimu katika kuimarisha utawala bora,” alisema.

Bw Maraga alisema ufisadi na kutekwa kwa asasi muhimu na wanasiasa na kumelemeza maendeleo.

“Ufisadi na vitendo vya ufisadi huendelezwa na wale ambao hawaheshimu sheria na kwa hivyo kupalilia umaskini. Kenya mhasibu mkuu wa serikali ameripoti kuwa thuluthi tatu ya bajeti ya taifa hupotea kupitia ufisadi,” alisema Bw Maraga.