Mapuuza ya sheria yaendelezwa na mawaziri

Mapuuza ya sheria yaendelezwa na mawaziri

Na CHARLES WASONGA

MOJAWAPO ya sababu zilizochangia mahakama kuu kuharamisha mchakato wa mageuzi ya Katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI) ni mazoea ya serikali ya kupuuza sheria.

Mapuuza hayo ya sheria na Katiba yamedhihirika tena baada ya mawaziri wa serikali wakiongozwa na Mutahi Kagwe (Afya) kuwashambulia hadharani majaji watano waliotoa uamuzi huo; na hivyo kuibua kero za Wakenya na wanasheria.

Hii ni kinyume na kanuni ya kikatiba ya utengano wa kimamlaka kati ya matawi matatu ya serikali inayosema kuwa tawi moja haliwe kuingilia utendakazi wa tawi jingine.

Vile vile, ni kinyume cha Katiba na sheria za utumishi wa umma kwa mawaziri kuingilia masuala ya kisiasa, kama vile mchakato wa BBI, unaoendeshwa na wanasiasa.

Akiongea katika kaunti ya Nyeri mwishoni mwa wiki jana, Bw Kagwe alitaja uamuzi huo kama pigo la muda tu huku akiwahakikishia Wakenya kwamba watapata mageuzi ya kikatiba wanayotaka mwaka huu au mwanzoni mwa 2022.

Waziri huyo wa Afya aliwaambia wananchi kutoingiwa na wasiwasi na wasibiri rufaa dhidi ya uamuzi huo huku wakiendelea kuvumisha yale aliyoyataja kama “mazuri yaliyomo kwenye Mswada wa BBI.”

“Kwangu sina shaka kwamba kwamba wakati kama huu mwaka ujao au mwishoni mwa mwaka huu tutakuwa na katiba mpya au iliyofanyiwa mageuzi,” Bw Kagwe akasema.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo Peter Munya alidai uamuzi wa majaji, Joel Ngugi, George Odunga, Chacha Mwita, Jairus Ngaah na Teresia Matheka, ulichochewa na chuki wala sio sheria na Katiba.

“Ni wazi kuwa walikuwa wakilipisha kisasi. Ikiwa unasaka kazi na ukakosa, jizuie na ukome kutumia cheo chako kulipisha kisasi,” akasema huku akionekena kuwarejelea Prof Ngugi na Bw Odunga. Hawa ni miongoni mwa majaji 41 ambao Raisi Uhuru Kenyatta alidinda kuwateua rasmi.

Watalamu wa masuala ya kisheria na Wakenya kwa ujumbla walimshutumu vikali waziri huyu wakisema kauli yake inaonyesha dharau kwa agizo la mahakama kwamba mchakato wa BBI unakiuka katiba na hivyo ni haramu na batili.

“Ni wazi kwamba Waziri Kagwe anaendeleza makosa yale yale ambayo serikali ya Jubilee imekuwa ikifanya kwa kupuuza maagizo au maamuzi ya mahakama. Amekiuka kipengele cha 159 cha Katiba kuhusu mamlaka ya Idara ya Mahakama kwa kupuuzilia uamuzi wa mahakama kuhusu BBI hata kabla ya suala hilo kuwasilishwa katika rufaa dhidi ya uamuzi huo,” akasema wakili Danstan Omari.

“Sharti mawaziri wa serikali waheshimu Katiba ambayo wao huapa kulinda na kuzingatia wanapoapishwa kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yao kulingana na kipengele cha 152 (4) cha Katiba,” akaongeza mwanasheria huyo.

Nao Wakenya mitandaoni walimkaripia Bw Kagwe, na wenzake wakisema mawaziri hao wametekwa na siasa kiasi cha kusahaua majukumu yao.

“Inaudhi kwamba Kagwe haheshimu mahakama. Akubali kuwa BBI ni haramu hadi mahakama ya rufaa itakapotoa uamuzi mwingi,” akasema Mwangi B, kupitia Twitter.

Naye Brigid @93 akauliza: “Kagwe ana kura ngapi za kupitisha mswada wa BBI?”

Kwa upande wake Mbunge wa Soy Caleb Kositany aliitaja serikali ya Jubilee kama sura halisi ya mapuuza ya sheria.

Katika uamuzi wao, majaji watano walisema mchakato wa BBI uliendeshwa kinyume cha Katiba na wakazima Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) dhidi ya kuandaa kura ya maamuzi kuhusu mswada wa marekebisho ya katiba.

You can share this post!

Mwanamume ajirusha kutoka orofa ya kumi Mombasa

Kocha Sam Allardyce kuagana rasmi na West Bromwich Albion...