Habari

Mapuuza yazua mauti shuleni

September 24th, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA

SHULE ya Msingi ya Precious Talents iliyo katika Wadi ya Ngando, eneobunge la Dagoretti Kusini ilikuwa sawa na mtego wa maafa kwa zaidi ya watoto 800, wataalamu wa masuala ya ujenzi wamesema.

Shule hiyo ya orofa moja iliyojengwa kwa mbao, mabati na nyaya bila vyuma, iliporomoka mwendo wa saa moja asubuhi jana na kusababisha vifo vya watoto saba waliokuwa darasani.

Watoto wengine 64 walipelekwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta ambapo wawili kati yao ndio waliopatikana na majeraha mabaya na wengine kuruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kutibiwa.

Katibu wa Taasisi ya Wahandisi wa Kenya, Bw Nathaniel Matalanga alisema ukaguzi wa vifusi vya shule hiyo ulionyesha kuwa hapakuwa na msingi thabiti, slabu (sakafu ya orofani) ilikuwa hafifu bila vyuma, na ukuta wa mabati haukufaa kwa jengo kama hilo.

“Ujenzi wa jumba haufai kufanywa namna hii. Lazima uchimbe msingi thabiti na ujenge ukuta unaoweza kushikilia uzito. Slabu inafaa kujengwa kwa kokoto. Hii ilikuwa kama inchi mbili hivi na badala ya vyuma, ilikuwa na waya kama wa kujengea kibanda cha kuku. Hata mtu anayejenga choo mashambani hawezi kamwe kujenga jinsi hii,” akasema.

Kisa hicho kilionyesha picha ya hali mbaya ambayo Wakenya wengi hupitia katika mitaa ya mabanda kote nchini wanakoishi.

Katika wadi hiyo ya Ngando, ilibainika hakuna shule yoyote ya umma wala hospitali ya umma. Shule pekee inayoweza kusemekana ni ya umma ni ile ya upili ya Lenana, ambayo ni shule ya kitaifa.

Wazazi na wananchi waliowasili eneo la mkasa kwa haraka kuokoa watoto, walilazimika kutegemea bodaboda kuwasafirisha hadi katika zahanati ndogo inayosimamiwa na Kanisa Katoliki ili kupokea huduma ya kwanza ya matibabu.

Baadhi ya wazazi walisema haingewezekana zahanati hiyo kuhudumia idadi kubwa ya watoto waliokuwa wakikimbizwa huko.

“Nilipompata mtoto wangu amejeruhiwa mguuni na kichwani, nilimchukua mara moja nikamweka kwenye pikipiki na kumkimbiza zahanati ya Katoliki lakini wahudumu wakaniambia hawataweza kumtibu. Nilibahatika kupata ambulensi ikamleta KNH,” akasema Bw Maurice Muthomi, mmoja wa wazazi.

Mbunge wa Dagoreti Kusini, Bw John Kiarie alisema wadi hiyo iliyo na idadi ya watu wapatao 30,000 haina ardhi ya umma ndiposa hakuna shule wala hospitali ya umma.

Ijapokuwa Waziri wa Elimu, Prof George Magoha alisema serikali itazingatia kujenga shule eneo hilo, kuna shule ya umma iliyo kilomita mbili pekee kutoka wadi hiyo ambayo watoto wanaweza kupelekwa.

“Serikali itajitahidi kuanzisha shule iwapo inahitajika. Suala la mipaka ya wadi halifai kuwa tatizo bali umbali wa shule kutoka mahali ambapo watoto wanaishi. Tutatafuta ardhi kwa njia yoyote ile na kujenga shule hapa miezi mitatu au minne ijayo,” akasema Prof Magoha.

Mmiliki wa shule hiyo, Bw Moses Wainaina, alidai kisa hicho kilisababishwa na mtaro wa maji-taka unaochimbwa karibu, ingawa hili halinwgethibitishwa.

Alisema shule hiyo huwa na wanafunzi karibu 800 kwa jumla na baadhi ya walioathirika walikuwa wakijiandaa kwa Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE) unaoanza mwezi ujao.