Michezo

Mara Sugar, Mathare ni bega kwa bega NSL

June 4th, 2024 2 min read

JOHN ASHIHUNDU Na ABDUL SHERIFF

VITA vya kuwania ubingwa wa taji la Supa Ligi (NSL) vinazidi kuchacha, lakini kulingana na msimamo wa ligi hiyo, Mara Sugar FC na Mathare United zinaendelea kubakia katika nafasi mbili za kwanza, kila moja ikibakisha mechi nne.

Baada ya kucheza mechi 38 nyumbani na ugenini, timu mbili zitafuzu moja kwa moja hadi Ligi Kuu ya Kenya (KFK-PL), huku timu itakayomaliza katika nafasi ya tatu ikikutana na itakayomaliza katika nafasi ya 16 katika mchujo wa kuwania nafasi nyingine ya kufuzu kwa ligi hiyo kuu.

Naivas inashikilia nafasi yatu ikiwa na pointi 64, mbele ya Nairobi United walio na alama 63 na mechi moja mkononi.

Mara Sugar wanaoongoza msimamo huo kwa pointi 75 waliibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Nairobi United katika mechi ngumu iliyochezewa Green Stadium, Awendo, Kaunti ya Migori wakifuatiwa na Mathare United walio na 71.

Katika mechi zao zilizobakia, Naivas watacheza na Nairobi United, Darajani Gogo, Mara Sugar na Mombasa Stars

Chini ya aliyekuwa kocha wa Harambee Stars, Francis Kimanzi aliyechukuwa nafasi ya Leonard Odipo aliyeondoka kwa hiari, Mathare United wana kibarua kigumu kulingana na mechi hizo.

Kisumu All Stars wanaokamata nafasi ya tano jedwalini waliikung’uta Darajani Gogo 1-0 katika mechi iliyochezewa KIHBT eneo la Ngong’ na kufikisha idadi ya pointi 59, wakati Dimba Patriots wakiibwaga Kajiado FC 3-2 ugani Ildamat Stadium, Kaunti ya Kajiado na kubakia katika nafasi ya 10.

Wakati huo huo, Mombasa Stars FC pekee kati ya timu tatu za Kanda ya Pwani ndiyo ambayo ishajinasua kubakia kwenye Supa Ligi (NSL) msimu ujao wakati Mombasa Elite FC na SS Assad FC zikiwa hatarini kuteremshwa ngazi.

Elite na Assad zilishindwa kwenye mechi zao walizochezwa viwanja vya nyumbani kwao mwishoni mwa wiki, Elite ikitandikwa 2-1 na Kibera Black Stars nayo Assad ikafungwa 1-0 na Luanda Villa 1-0.,

Matumaini ya Mombasa Stars ya kufikia nafasi ya saba hayakufaulu baada ya kutoka sare ya 1-1 na Rainbow lakini imebakia nafasi nzuri ya kuwahakikishia kubakia ligi kwa kuwa kwenye nafasi ya tisa ikiwa na pointi 47.