Afya na Jamii

Ukosefu wa maji safi wasababisha ongezeko la maradhi ya ngozi

June 8th, 2024 2 min read

NA ANTHONY KITIMO

UHABA wa maji katika Kaunti ya Kilifi unaendelea kusababisha maradhi ya ngozi kwa wakazi kama ilivyodhihirishwa katika kambi ya matibabu eneo la Ganze.

Mamia ya wakazi wa Ganze walitambuliwa kuathirika na maradhi ya ngozi kutokana na ukosefu wa maji safi katika kambi ya matibabu iliyosimamiwa na Hospitali ya Tudor Healthcare.

Mkurungenzi mkuu wa Tudor Healthcare Dkt Tobias Khoi, alisema wagonjwa wengi haswa watoto na wazee walipokea matibu ya ngozi pamoja na ya magonjwa mengine mengi.

“Eneo la Ganze ni eneo kame hivyo basi uhaba wa maji ni jambo linashuhidiwa na kusabisha magojwa mengi hasa kwa watoto na wazee. Pia wanawake wameathiriwa na shida hiyo haswa katika sehemu zao za siri,” alisema Bw Khoi.

Akiongea eneo la Ganze, Dkt Khoi alisema Tudor Healthcare walichagua eneo hilo ili kupeleka huduma za matibabu nyanjani.

“Kaunti ya Kilifi tuko na matawi mengi ya hospitali ya Tudor Healthcare lakini ukosefu wa matibabu muhimu umetufanya kupeleka kambi ya matibabu eneo hilo. Kama hospitali, tutaendelea kutoa huduma hizo na waliotibiwa na kupatikana na magonjwa ambayo hayangeweza kutibiwa hapo, tumeowaomba kutembelea kitu chetu chochote kwa matibabu zaidi,” alisema Dkt Khoi.

Bi Rahma Penda, mkazi wa Ganze, alisema iko haja ya kupanga kambi hizo za afya kila wakati kwani zinapunguza garama ya kutafuta huduma hizo. “Huwa inatupasa kutembea muda mrefu hadi katika zahanati zilizoko eneo hili na kwa muda mwingi tunapata hakuna dawa ama wahudumu wakutosha hivyo basi zoezi la leo limekuwa la kufana sana,” alisema Bi Penda.

Akiongea wakati wa kuidhinisha msafara wa hospitali ya Tudor Healthcare kutoa huduma hizo eneo la Mariakani, mwakilishi wadi wa eneo hilo Martha Koki, aliomba wahisani waendelee kutoa huduma hizo bila kusita.

Bi Koki alisema sehemu nyingi za Kaunti ya Kilifi zinakumbwa na changamoto kadhaa hivyo basi ni jambo la kutia moyo kuona mashirika mbali mbali kusaidia wakazi hao.

“Leo tunaelekea Ganze lakini tunaomba washirika kupitia afisi yangu kushirikiana kutoa huduma hizo katika sehemu nyingi, ikiwemo wadi ya Mariakani,” alisema Bi Koki.

Hata hivyo alisema kama kiongozi wa wadi, atashinikiza serikali kuu na ile ya Kaunti kutenga fedha za kutosha kukimu kahitaji ya wakazi hao.

“Kuna shida ya chanjo za watoto pamoja na uhaba wa dawa mbalimbali ndio maana tunaomba siku za usoni, tuhakikishe dawa zinaletwa katika zahanati mashinani,” alisema.