Makala

Maradhi ya zinaa yazidi Thika, wengi wakilaumiwa kupuuza kondomu

May 3rd, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

WENYE mazoea ya kushiriki starehe za kimwili bila kinga wameonywa kwamba visa vya maambukizi ya magonjwa ya zinaa vimeongezeka mjini Thika.

Kwa mujibu wa ripoti ya hivi punde, kisonono, kaswende na malengelenge ni baadhi ya maradhi ambayo yanasambaa kwa wingi katika eneo hilo.

Mji wa Thika husifika kwa kuwa ngome ya vibiritingoma ambao hujichuuza kwa kila kona kwa wakati wowote ule wa mchana na usiku wakitumia kila aina ya mbinu ya kuchumbia wanaume.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Aids Healthcare Action Foundation (AHAF), waliopimwa na kugunduliwa walikuwa wameathirika na maradhi ya zinaa eneo hilo kati ya Januari 1, 2024, hadi Aprili 30, 2024, ni watu 1,432.

Kati yao walikuwa ni wanaume 489 hao wengine 943 wakiwa ni wanawake.

Takwimu hizo ni zile zilizokusanywa kutoka hospitali za eneo hilo ambazo hushirikiana katika mikakati ya kuhudumia walio katika hatari za magonjwa ya zinaa.

“Idadi hiyo kubwa ya wanawake kuwa na magonjwa hayo ya zinaa na pia kuambukiza idadi hiyo ya wanaume inaashiria matumizi ya mipira ya kondomu yamepuuzwa. Ina maana kwamba wanawake wengi walio katika biashara hiyo wana maradhi ya zinaa na pengine hawajui hivyo wanazidi kuchoma wateja wao,” ripoti hiyo yasema.

Mkurugenzi wa AHAF, Leah Muchoki aliambia Taifa Leo kwamba uchunguzi kupitia mahojiano na wagonjwa hao umebaini kwamba wengi wao hushiriki katika biashara hiyo wakipendelea kuonana bila kinga kwa kuwa huwa wanatumia dawa za kukinga maambukizi ya virusi vinavyosababisha Ukimwi (VVU au HIV).

“Kuna dawa ambazo washiriki wa tendo la kurushana roho humeza kabla–ambayo ni Pre-Exposure Prophylaxis (PrEP)–na nyingine ya baada ya kuonana ijulikanayo kama Post-Exposure Prophylaxis (Pep) na ambayo nia kuu ni kuzima maambukizi ya VVU au HIV. Ina maana kwamba washirika katika biashara hii huogopa tu Ukimwi lakini wakijitosa katika hiyo bahari ya kurushana roho, wanajipata wamejizolea kisonono na kaswende,” akasema Bi Muchoki.

Aliongeza kwamba kuna shida nyingine ambayo kidole cha lawama anaelekeza kwa serikali, ya uhaba wa mipira ya kondomu nchini.

“Hiii imekuwa kero kuu katika biashara hiyi na ndipo wengi wakisaka njia za kujinusuru hutumia hata karatasi za nailoni zilizopigwa marufuku na pia kukumbatia sayansi hiyo ya kumeza dawa ya kuzima makali ya Ukimwi,” akasema.

Mmoja wa wanakamati wa muungano wa wanawake hao wa Thika Bi Anne Wambui alisema kwamba “bila kondomu malipo huwa ya juu na unapata wateja wengi, hivyo basi wengi kuamua bora tu sio Ukimwi ambao hauna dawa, hayo mengine ya magonjwa yatakimbizwa tu hospitalini na yatibike”.

Alisema kwamba magonjwa hayo mengine ni athari tu za kibiashara.

Mshirikishi wa matumizi ya kondomu nchini Bi Brenda Alwanyi, alisema kwamba “kuna haja kubwa kwa serikali kugundua kwamba kuna pengo la usambazaji mipira hiyo nchini na ambalo linaleta kila aina ya madhara”.

“Kila mwaka ni lazima kutolewe ripoti za uhaba wa kondomu na pia habari za jinsi zile kidogo zilizoko zimeibwa na mabwanyenye wa kuwekeza katika siasa na biashara,” akasema Bi Alwanyi.

Yule anayetambulika kama mfalme wa kondomu barani Afrika Bw Stanley Ngara, alisema kwamba shida kuu ya ukosefu wa mipira na ongezeko la magonjwa ni ukosefu wa utekelezaji sera.

“Kila kitengo cha serikali kinaelewa kuhusu sera zilizowekwa za kupambana na madhara ya magonjwa ya zinaa. Lakini ikiwa mikakati ya uhamasisho imetelekezwa, ufadhili kuzidi kumezwa pasipo kuafikia malengo yaliyokusudiwa pamoja na wizi hata wa kondomu ukiendelea kushuhudiwa, basi tusilie mbona hali iko hivyo,” akasema Bw Ngara.