Michezo

Maradona afurusha mchumba mpenda starehe kupindukia

January 28th, 2019 1 min read

NA CHRIS ADUNGO

NGULI wa soka ya Argentina, Diego Maradona, 58, ameapa kumfurusha mchumba wake Rocio Oliva katika kasri lake jijini Buenos Aires jijini Argentina na hata kulitwaa jumba la kifahari alilowanunulia wazazi wa kichuna huyo aliyetemana naye miezi sita iliyopita.

Pamoja na hayo, Maradona ambaye kwa sasa ni mkufunzi wa kikosi cha Dorados de Sinaloa amefichua mipango ya kumshtaki Rocio kwa madai ya kufuja fedha za dume lake kwa kuandaa safari nyingi zisizo na maana kwa lengo la kuponda raha ya ujana.

“Mimi si mpenda vita na haikuwa nia yangu kumpiga Rocio kiasi cha kutaka sana kumdumua kichwa miezi sita iliyopita kutokana na ukubwa wa makosa aliyonifanyia,” alisema Maradona kwa kufichua kiini cha kutemana kwake na kipusa huyo mwenye umri wa miaka 28.

Mwaka jana, Maradona alizua kizaazaa katika mojawapo ya vyumba vya wageni katika hoteli ya Eurostars Suites Mirasierra jijini Madrid, Uhispania kwa kugombana na demu wake Rocio. Kwa mujibu wa Oliva, ugomvi kati yake na Maradona ulitokana na hatua ya veterani huyo wa soka kudai fursa ya kurejea tena mzingani mwake kurina asali wakati ‘usiofaa’.

Gazeti la The Sun lilidai hatua ya Rocio kumnyima Maradona tunda lake majira ya saa mbili na nusu asubuhi ilimkasirisha sana mwanasoka huyo wa zamani na hivyo akashindwa kuzidhibiti kabisa hasira zake.

“Alinikwida kabisa na kwa mara ya kwanza sikuelewa kusudi lake. Nadhani hisia zilikuwa zimezidia nami wakati huo nikiogopa kumruhusu tena kurejea mzingani kwa hofu ya ‘kuwasumbua’ wageni wengi waliokuwa katika hoteli ya Eurostars wakisubiri kutazama mechi fulani ya KlabuBingwa Ulaya (UEFA),” alikiri Rocio.

Iliwalazimu maafisa wa polisi kuitwa kuingilia kati na kuuzima ugomvi kati ya Maradona na kidosho wake.