Kimataifa

Maradona kuzikwa Disemba 3 katika makaburi ya Jardin de Paz nchini Argentina karibu na walikozikwa wazazi wake

November 28th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

BUENOS AIRES, Argentina

ALIYEKUWA nguli wa soka nchini Argentina, Diego Maradona atazikwa viungani mwa jiji la Buenos Aires mnamo Disemba 3, 2020.

Maradona aliaga dunia mnamo Novemba 25, 2020 kutokana na mshtuko wa moyo akiwa na umri wa miaka 60. Mazishi yake yatafanyika katika makaburi ya Jardin de Paz nchini Argentina, ambako wazazi wake walizikwa.

Haya ni kwa mujibu wa Sebastian Sanchi ambaye ni msemaji wa familia ya mwendazake.

Meya wa jiji la Naples nchini Italia tayari amependekeza uwanja wa Stadio San Paolo ubadilishwe jina na kuitwa Diego Maradona kwa heshima ya jagina huyo wa soka aliywahi kuchezea kikosi cha Napoli katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

“Naomba uga wa San Paolo sasa uitwe Dirgo Armando Maradona!” akasema Meya Luigi de Magistris kupitia mtandao wake wa Twitter.

Katika enzi yake ya usogora, Maradona aliongoza Napoli kutia kapuni mataji mawili ya Serie A mnamo 1987 na 1990.

“Diego alitufanya kuzinduka ndotoni. Aliwasha mwenge wa matumaini jijini Naples na akatuletea furaha na tija kwa kiwango sawa ambacho Argentina nayo iliona fahari kuwa naye kikosini mwao,” akaongeza Magistris katika kauli iliyoungwa mkono na mmiliki wa Napoli, Aurelio De Laurentiis.

Kwa heshima ya Maradona, Napoli watatumia uwanja wa San Paolo kusakata gozi la Europa League dhidi ya Rijeka usiku wa Novemba 26, 2020.