Habari

Maraga adokeza atang’atuka mapema

July 1st, 2020 2 min read

Na VALENTINE OBARA

JAJI Mkuu David Maraga, amedokeza ataondoka afisini mapema kabla astaafu mwaka 2021.

Kustaafu kwa Jaji Maraga atakapohitimisha umri wa miaka 70 Januari, kumekuwa kukiibua mdahalo mkali miongoni mwa wanasiasa na washikadau katika sekta ya haki.

Hii ni ni kwa kuwa, atakayechukua mahala pake atakuwa na jukumu kubwa wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao endapo kutatokea malalamishi kuhusu matokeo ya kura za urais.

Akizungumza Jumatano wakati wa kuzindua wa mfumo wa kidijitali utakaotumiwa kuwasilisha na kuhifadhi stakabadhi za kesi Nairobi, jaji mkuu alisema anafahamu wazi kwamba, umri wake umekuwa mkubwa na hivyo basi muda wake wa kustaafu umekaribia.

“Kwa kawaida Jaji anayestaafu huhitajika kuchukua likizo ndefu kabla muda wake wa kustaafu ufike. Kwa hivyo, wakati wangu ukifika, nitapewa barua na Msajili wa Mahakama niende likizo. Nadhani hilo litafanyika Novemba lakini kwa sasa bado nipo,” akasema.

Aliibua ucheshi alipofafanulia waliohudhuria hafla hiyo kuhusu umri wake mkubwa kwa kusisitiza kinasa sauti kifukiziwe dawa vyema ili ajiepushe kuambukizwa virusi vya corona.

“Nilitaka nifukiziwe dawa hapa kwa maikrofoni vizuri kwa sababu wengi wenu mmezungumzia umri wangu na mnafahamu kile ninamaanisha. Nashukuru wale wamenitakia mema,” akasema.

Jaji Mkuu aliyemtangulia, Dkt Willy Mutunga, alienda likizo kama hiyo mwaka mmoja kabla muda wake wa kustaafu akisema alitaka serikali ipate muda wa kutosha kujaza nafasi yake.

Uhusiano kati ya mahakama na Ikulu ulidorora wakati Jaji Maraga alipoweka historia Afrika kwa kusimamia kikao cha Mahakama ya Juu kilichofutilia mbali ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa 2017 ambao ulikumbwa na dosari tele.

Wakati huo, Rais Kenyatta na wandani wake katika Chama cha Jubilee waliapa ‘kuifunza adabu’ Idara ya Mahakama na kufikia sasa kumekuwa na mivutano kati ya asasi hizo mbili za serikali.

Jaji Maraga huwa hafichi kuchukizwa kwake na jinsi mahakama inavyopunguziwa bajeti. Mvutano wa hivi majuzi ulihusisha jinsi Rais alichelea kuteua majaji 41 waliopitishwa na Idara ya Huduma za Mahakama (JSC) licha ya kuagizwa kufanya hivyo na mahakama.

Kwa kumtetea Rais, Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki alidai serikali ilikuwa imekata rufaa dhidi ya uamuzi huo kwani Ikulu inaamini baadhi ya majaji kwenye orodha hiyo si waadilifu.

“Wakati mwingine huwa naona magazeti yakisema ninalia. Nitaendelea kulia kwa minajili ya haki za Wakenya,” akasema.

Alisisitiza kuwa, mpango muhimu aliozindua jana ulifadhiliwa na shirika la International Development Law Organization (IDLO).

Katika mpango huo ambao kwa sasa utatumiwa katika Mahakama ya Juu, Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu Nairobi, stakabadhio zote za kesi zitahitajika kuwasilishwa mtandaoni.

Jaji Maraga alisema mahakama imeweka mipango kuhakikisha utumizi wa mbinu za kidijitali hautabagua wale wasio na uwezo wa kutumia mitandao ya intaneti.

Kwa mfano, alitangaza mpango wa kuwezesha watu kufuatilia kesi zao kwa kutuma nambari ya kesi kwa simu, kisha wafahamishwe badala ya kusafiri hadi mahakamani.