Habari

Maraga afichua jinsi alivyotishwa mara kadha

December 17th, 2020 2 min read

Na DIANA MUTHEU

JAJI Mkuu, David Maraga katika mkutano wake wa mwisho na majaji pamoja na mawakili katika mahakama kuu ya Mombasa, Alhamisi amefichua kuwa alipokea vitisho mara kwa mara kutoka kwa watu ambao hawakufurahishwa na baadhi ya maamuzi yake ya ujasiri wa hali ya juu.

Hata hivyo, alisema vitisho hivyo havikumnyima usingizi, kwa kuwa alikuwa kila usiku akilala akiwa anajua alikuwa ameifanya kazi yake kwa mujibu wa sheria, chini ya mwongozo wa katiba ya Kenya, na bila mapendeleo au kujihusisha katika ufisadi wa aina yoyote.

“Furaha yangu kubwa ni kuwa Wakenya walinitetea. Picha za utani zilisambazwa kote mitandaoni, sikujibu wala hakuna mtu yeyote ofisini mwangu alijibu. Wakenya walijibu kwa niaba yangu na ninawashukuru sana,” amesema Jaji Maraga huku akidinda kutaja baadhi ya matukio yaliyomfanya apate vitisho hivyo, na akawaomba mawakili na majaji wazingatie ukweli na kufanya kazi zao kwa mujibu wa Katiba bila kuogopa vitisho.

Hata hivyo, katika kumbukumbu za matukio kwa kipindi cha miaka minne akihudumu kama Jaji Mkuu, Bw Maraga atakumbukwa kwa kuongoza jopo lililofutilia mbali uchaguzi wa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto mnamo mwaka wa 2017, kutokana na hitilafu za matokeo ya kura za urais.

Zaidi, jaji mkuu huyo ambaye ni wa 14 humu nchini alizua gumzo la kitaifa alipomtaka Rais kuvunja Bunge la Kitaifa kwa kushindwa kutekeleza sheria ya usawa wa jinsia.

Alizungumzia hayo Mombasa, mahali ambapo alihudumu kwa mara ya kwanza kama jaji wa mahakama Kuu kuanzia mwaka wa 2003 hadi 2008 kabla ya kuhamishwa hadi Nairobi.

“Nina furaha kuzuru ofisi yangu ambapo nilifanya kazi ya ujaji kwa mara ya kwanza kabisa. Hii ni kumbukumbu ya kazi nzuri ambayo tulifanya. Nikianza kazi yangu kulikuweko na majaji watatu tu na mawakili 150 wakihudumu katika eneo hili. Sasa nina furaha kuwa idadi imeongezeka. Kwa sasa kuna majaji 11 na mawakili zaidi ya 600 wanaosaidia Wakenya kupata haki,” akasema.

Katika hafla hiyo ambayo ilitajwa kama Mazungumzo ya Mwisho yaani The Last Conversations, Jaji Mkuu alipambwa kwa sifa mbalimbali na majaji, mawakili na hata watumizi wa korti, baada ya kuanza likizo ndefu kabla ya kustaafu kwake mnamo Januari, 2021 atapokuwa anatimiza umri wa miaka 70.

Jaji Eric Ogola ambaye aliongoza hafla hiyo, alimtaja jaji Maraga kuwa mtendakazi na kusema kuwa watahakikisha wanafuata nyayo zake katika utendakazi wao.

“Tunamshukuru Jaji Mkuu kwa kuwa mfano mwema katika uongozi wake. Tunaahidi kufuata msingi huo huo,” akasema jaji Ogola.