Habari Mseto

Maraga ahimiza vituo vya polisi vikumbatie mfumo wa kidijitali

March 19th, 2019 2 min read

NA CECIL ODONGO

JAJI Mkuu David Maraga Jumatatu aliipa changamoto Tume ya Huduma za Polisi(NPSC), kufanikisha utaratibu wa matumizi ya njia za kielektroniki za kusajili nakala za mashtaka katika sajili ya mahakama, ili kutochelewesha kesi zinazowasilishwa kortini.

Bw Maraga alisema NPSC ina jukumu la kuhakikisha tatizo la washtakiwa kuzuiliwa kwa saa kadha kutokana na ukosefu au uwepo wa dosari kwenye nakala ya mashtaka linatatuliwa kupitia teknolojia ya kisasa.

Jaji mkuu huyo alisema hayo jana alipoongoza hafla ya kuapishwa kwa Makamishna sita wapya wa NPSC.

Bw Maraga alisema tume hiyo italazimika kushauriana na serikali kuu ili kutafuta jinsi maeneo yanayokosa umeme yatakumbatia mpango huo mpya unaolenga kurejesha matumaini ya raia kwa polisi na mahakama.

Makamishna walioapishwa ni Mwenyekiti Eliud Kinuthia, wanachama Lilian Kiamba, Eusibius Laibuta, Naftali Kipchirchir Rono, Alice Atieno Otwala na John Ole Mayaki.

“Inasikitika kwamba polisi bado wako nyuma sana ukizingatia namna suala la nakala za mashtaka hata zile za kesi kubwa linavyotumiwa kukiuka haki za raia na kupiga breki mchakato wa upatikanaji wa haki,” alisema.

Aliongeza, “Tunafaa kutumia teknolojia ya kielektroniki kuhakikisha mashtaka katika kituo cha polisi yanafikia kitengo chetu cha usajili ili kuzuia kesi kuchelewesha bila sababu za kuridhisha.”

Jaji Mkuu aliwataka makamishna hao kujikita sana kuhusu jinsi ya kuimarisha maisha ya polisi na masuala wanayokumbana nayo wakiwa kazini.

“Naomba tume hii ihakikishe polisi wanaofikishwa mbele yao kwa kukiuka maadili ya kazi wanasikizwa na uamuzi unaofaa kutolewa. Tusiwadhulumu polisi ilhali wao ndio hudhibiti sekta muhimu ya kiusalama nchini,” akaongeza Bw Maraga.

Mwenyekiti mpya, Bw Eliud Kinuthia alisema tume yake imeandaa orodha ya hoja muhimu itakayojizatiti kumaliza kwa muda wa siku 100 ofisini. Hoja hizo zinalenga kuimarisha utendakazi wa maafisa wa polisi kwa kuangazia maslahi yao.

“Tutatumia tajriba na ujuzi wetu kukabiliana na changamoto zinazowaathiri polisi na pia kutimiza matarajio ya umma. Tuna malengo muhimu ya kutimiza ndani ya siku 100 na tunaomba ushirikiano na uungwaji mkono,” akasema Bw Kinuthia anayechukua nafasi hiyo kutoka kwa Johnstone Kavuludi.