Habari Mseto

Maraga akiri majaji wamezembea kuamua kesi

August 19th, 2019 1 min read

Na MISHI GONGO

JAJI Mkuu David Maraga Jumatatu alikiri idara anayosimamia inajikokota katika kuamua kesi.

Hii ni baada ya lawama ambazo zimekuwa zikielekezewa Idara ya Mahakama kwa kuchelewesha utatuzi wa kesi.

Akihutubia majaji jana jijini Mombasa, Jaji Maraga alitaja Mahakama ya Rufaa kama iliyolemewa zaidi kwa kuchukua miaka mitatu kuamua kesi moja.

“Kesi ya uhalifu inayokamilishwa haraka zaidi na Mahakama ya Rufaa huchukua siku 1,235 ambayo ni sawa na miaka mitatu, huku Mahakama Kuu ikichukua siku 522 kuamua kesi ambayo ni sawa na mwaka mmoja na nusu,” akasema Bw Maraga.

Alisema katika mahakama inayoshughulikia masuala ya leba, kesi inayoharakishwa zaidi huchukua zaidi ya miaka miwili, ilhali katika mahakama ya ardhi na mazingira huchukua miaka mitatu.

“Ijapokuwa takwimu hizi zinaonyesha mabadiliko makubwa ikilinganishwa na mwaka uliopita, bado juhudi zaidi zinatakikana kupunguza hali hii,” akasema Jaji Maraga.

Alizipongeza mahakama za mahakimu akisema ndizo huchukua muda mfupi zaidi kuamua kesi zao ingawa bado zinachukua zaidi ya mwaka mmoja.

Alisema licha ya changamoto zilizopo, kuna mabadiliko makubwa ya uamuzi wa kesi ikilinganishwa na mwaka uliopita, ambapo kulikuwa na kesi zaidi ya 110,000 ambazo zilikuwa zimesalia mahakamani kwa muda wa zaidi ya miaka mitano.

Alisema kesi hizo zimeamuliwa na zimesalia 15,278 pekee.

Alieleza matumaini kuwa matumizi ya teknolojia katika korti yatasaidia kumaliza kucheleweshwa kwa uamuzi wa kesi.