Habari

Maraga amkaribisha kinara mpya wa PSC kusaidia kutatua kesi za ardhi

August 15th, 2018 2 min read

Na PETER MBURU

JAJI Mkuu David Maraga amemkaribisha mwenyekiti mpya wa Tume ya Huduma za Umma (PSC) Bw Stephen Kirogo kwa wito kuwa aanze kazi kwa kushinikiza mabadiliko kwenye sekta ya ardhi, ambayo alisema imesababisha msongamano wa kesi kortini.

Bw Maraga alisema nyingi za kesi zilizosongamana kwenye mahakama za humu nchini kwa miaka mingi zinahusiana na masuala ya ardhi, akisema sasa maafisa wa idara yake wanakumbwa na wakati mgumu kuzitatua.

Kulingana na Bw Maraga, pengo kwenye taasisi za kusimamia masuala ya ardhi zimesababisha kuongezeka kwa kesi hizo, kwani sasa matapeli wanaweza kupata hati za umiliki wa mashamba kwa kushirikiana na maafisa wa ardhi, hivyo akimtaka Bw Kirogo kuidhinisha mabadiliko yatakayosaidia taifa.

“Shida nyingi tulizonazo katika idara ya mahakama zinatokana na masuala ya ardhi, tuna kesi ambapo shamba moja lina hati mbili ama tatu za umiliki na tunahangaika kubaini nani haswa mmiliki wa shamba kama hilo,” akasema Bw Maraga.

“Nimekutana na watu wanaoishi nje ya nchi na ambao wangependa kuwekeza humu nchini. Wengine walienda kwenye afisi za ardhi na kufuata mikondo ya ununuzi wa shamba kabla ya kulipa lakini walipotaka kujenga, wanapata wengine wakiwa na hati za umiliki kama wao,” akasema Jaji Mkuu.

Akizungumza katika mahakama ya juu Jumatano wakati wa kuapishwa kwa Bw Kirogo, Bw Maraga alisema hata baadhi ya benki zimeenda hasara baada ya kukopesha kisha zinapotaka kunadi mashamba ya waliokopa zinapata wamiliki wengine walio na hati za umiliki.

Mkuu wa utumishi wa umma Joseph Kinyua alimpa changamoto Bw Kirogo, ambaye amefanya kazi ya utumishi wa umma kwa zaidi ya miaka 30, kuwa utendakazi wa idara hiyo unaadhiri taswira ya taifa nje na ndani.

“Hauhitaji kuendesha magari yote makubwa kwa kuwa umepewa nafasi hii, hii ni nafasi kuboresha taifa letu,” akasema Bw Kinyua.

Bw Kirogo alieleza matumaini yake kuwa atafanya awezalo kuidhinisha mageuzi ya umuhimu kwa taifa katka sekta ya utumishi wa umma.

“Ninafahamu hata kufaulu ama kufeli kwa malengo manne makuu ya serikali kutategemea utendakazi wa sekta hii. Nitahakikisha kuwa wafanyakazi wa umma wanafanyia kazi mshahara ila si kulipwa bure tu,” akasema Bw Kirogo, baada ya kuapishwa.