Habari Mseto

Maraga amwelekezea DPP lawama kuhusu ufisadi

December 17th, 2018 1 min read

Na COLLINS OMULO

JAJI Mkuu David Maraga ameilaumu afisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) kwa kuchelewesha kukamilika kwa kesi za ufisadi nchini.

Bw Maraga alisema kuwa kesi hizo zimekuwa zikichukua muda mrefu kwani afisi hiyo huwa haiwasilishi stakabadhi muhimu kama inavyohitajika na mahakama, ili kuharakisha kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi hizo.

Bw Maraga alisema kuwa kesi nyingi huwa zinaanza hata wakati ambapo afisi hiyo haijapata stakabadhi muhimu, hali ambayo huchangia nyingi kuahirishwa ili kutoa muda wa ushahidi zaidi kukusanywa.

“Anapoanza baadhi ya kesi, DPP NoordinHaji huwa hana stakabadhi zote. Hata hivyo, tumemwambia kuanza kesi akiwa na stakabadhi zote ili kuepuka hali ambapo kesi husika zinaahirishwa mara kwa mara. Wanashughulikia hilo,” akasema Bw Maraga.

Alitoa kauli hiyo akihutubu jana katika Gereza la Kamiti, kwenye ziara iliyoandaliwa na Kanisa la Seventh Day Adventist (SDA).

Kauli ya Bw Maraga inajiri baada ya Idara ya Mahakama kulaumiwa kutokana na kiwango cha chini cha dhamana ambacho imekuwa ikiwapa washukiwa wakuu wa ufisadi.

Lawama hizo zimetolewa na Rais Uhuru Kenyatta na Bw Haji.

Rais alitoa malalamishi hayo Jumatano iliyopita kwenye maadhimisho ya Sikukuu ya Jamhuri, akiionya idara hiyo kwamba viwango hivyo vya dhamana vinarejesha nyuma vita dhidi ya ufisadi.

“Kwa mara nyinyine, ninaiomba Idara ya Mahakama kuhakikisha kwamba kanuni zake hazitumiki kuwalinda wakwepaji adhabu. Wakenya wanapoteza matumaini wanapowaona washukiwa wa ufisadi wakiachiliwa kwa dhamana ndogo au kucheleweshwa kwa kesi zinazowakabili,” akasema Rais Kenyatta.

Kauli ya Rais ilijiri baada ya Bw Haji kusema kuwa anatatizika kiutendakazi katika kesi zinazowakumba maafisa wakuu wa serikali walio mamlakani na wanaoendelea kupokea mshahara.