Habari Mseto

Maraga arukwa katika uteuzi wa Jaji Nyachae

February 25th, 2018 2 min read

Bw Charles Nyachae aliyeteuliwa jaji kuwakilisha Kenya katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ). Picha/ Maktaba

Na WALTER MENYA

Kwa ufupi:

  • Idara ya Mahakama ilikuwa imempendekeza Jaji Hannah Okwengu katika cheo hicho
  • Taifa Jumapili imepata barua kati ya Wizara ya Masuala ya Afrika Mashariki na idara hiyo, ambapo Jaji Mkuu David Maraga alimpendelea Bi Okwengu
  • Bw Nyachae alimfanyia kampeni Rais Kenyatta na Chama cha Jubilee katika Kaunti ya Kisii, kwenye chaguzi za Agosti 8 na Oktoba 26

SERIKALI Kuu ilipindua pendekezo la Jaji Mkuu Jaji Maraga, kuhusu jaji aliyefaa kuwakilisha Kenya katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ), imefichuka.

Imebainika Idara ya Mahakama ilikuwa imempendekeza Jaji Hannah Okwengu katika cheo hicho, lakini badala yake jina la Bw Charles Nyachae, aliyeteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta ndilo likatumwa.

Hata hivyo, serikali ilipuuzilia mbali pendekezo la idara hiyo na badala yake kumteua Bw Nyachae.

Mwenyekiti huyo wa zamani wa Tume ya Utekelezaji Katiba (CIC) aliapishwa rasmi mnamo Ijumaa, jijini Kampala, Uganda ambapo alichukua nafasi ya Jaji Isaac Lenaola.

Kipindi cha kuhudumu cha Bw Lenaola kitaisha mnamo Julai 1.

Aidha, Taifa Jumapili imepata barua kati ya Wizara ya Masuala ya Afrika Mashariki na idara hiyo, ambapo Jaji Mkuu David Maraga alimpendelea Bi Okwengu.

“Jaji David Maraga, aliye pia Mkuu wa Mahakama ya Juu ya Kenya amependekeza Jaji Okwengu kuwa kuhudumu katika mahakama ya EACJ,” akasema Bi Anne Amandi, ambaye ni Msajili wa Idara ya Mahakama, iliyoandikwa mnamo Februari 14.

Barua ya Bi Amadi ilikuwa majibu ya barua ya Wizara hiyo mnamo Desemba 22, 2017 ikiiomba Idara ya Mahakama kumpendekeza mtu atakayeteuliwa kuhudumu katika mahakama hiyo. Barua ya wizara ilitiwa saini na Dkt Alice Yalla, kwa niaba ya Katibu wa Wizara.

 

Amsaidia Rais kwa kampeni

Bw Nyachae alimfanyia kampeni Rais Kenyatta na Chama cha Jubilee katika Kaunti ya Kisii, kwenye chaguzi za Agosti 8 na Oktoba 26.
Mbali na hayo, aliwania useneta katika kaunti hiyo kwa tiketi ya JP.

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili nchini (LSK) anayeondoka, Bw Isaac Okero, alisema: “Mwafaka wa Muungano wa Afrika Mashariki (EAC) ni mojawapo ya sheria zetu.

Unasema kwamba kuna utaratibu unaopaswa kuzingatiwa katika uteuzi wa majaji katika EACJ. Kulingana na taratibu zilizopo, mtu huyo anapaswa kupendekezwa kwa rais na Tume ya Huduma za Mahakama, hilo likimaanisha kuwa lazima mchakato wa uteuzi uwe wenye uwazi.”

Naye mwenyekiti wa zamani wa LSK, Bw Eric Mutua, anasema kuwa, hatua hiyo ni ishara ya wazi kwamba Idara ya Mahakama imenyang’anywa mamlaka yake.