Habari Mseto

Maraga ashauri Uhuru kuvunja Bunge la Kitaifa

September 22nd, 2020 2 min read

BENSON MATHEKA na CHARLES WASONGA

JAJI Mkuu David Maraga, sasa amewaweka Wabunge katika hatari ya kupoteza viti vyao ikiwa Rais Uhuru Kenyatta atakubaliana na pendekezo lake la kuvunja Bunge kwa kukiuka Katiba.

Pendekezo hilo lililotolewa Jumatatu linaonekana na wadadisi kuwa kubwa la mwisho ambalo Jaji Maraga ametoa kabla aelekee likizoni hivi karibuni kisha astaafu ifikapo Januari 2021.

Wito wa kuvunja Bunge ulitoka kwa mashirika mbalimbali kwa kushindwa kupitisha sheria ya kuhakikisha usawa wa jinsia.

Kwenye barua aliyomwandikia Rais Kenyatta, Bw Maraga alisema alifikia uamuzi wa kumshauri avunje Bunge baada ya kupokea maombi sita kutoka kwa Wakenya wakimtaka afanye hivyo.

“Malalamishi katika maombi haya sita yaliyo mbele yangu ni kuwa bunge kwa miaka tisa na maagizo manne ya mahakama ikiwa ilishindwa kupitisha sheria ya kutekeleza usawa wa jinsia, ninafaa kukushauri uvunje Bunge,” anamweleza Rais.

Anasema kwamba, kwa vile bunge halikumfahamisha iwapo lilipitisha sheria hiyo, aliwaita maspika wawili na Mwanasheria kwa mkutano mnamo Agosti 3, 2020, ambao walipuuza maombi hayo wakisema hayakuwa yametoka katika Mahakama Kuu.

Bw Maraga anasema kwamba, maspika walimweleza kwamba hakuwa na mamlaka ya kuchukua hatua wakisema ni jukumu la Mahakama Kuu kufasiri katiba.

“Kinyume na kauli za maspika, katiba inampatia Jaji Mkuu mamlaka ya kumshauri rais kuvunja Bunge. Hata hivyo katiba haimruhusu Jaji Mkuu kuandaa kikao cha kusikiliza ombi au pingamizi,” alisema.

Lakini kulingana na spika wa Bunge Justin Muturi, Bunge halifai kulaumiwa kwa kukosa kupitisha sheria hiyo.

Bw Muturi alisema ni jukumu la serikali kuu kufanikisha usawa wa jinsia na kwamba, hakuna sheria inayolazimisha Bunge kupitisha sheria hiyo.

Alipendekeza suala hilo lishughulikiwe katika Mpango wa Maridhiano (BBI) unaolenga kubadilisha katiba.

Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) pia ilipinga pendekezo la Bw Maraga.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Muturi Kigano alisema Jumatatu hatua hiyo italemaza majukumu ya serikali kijumla.

“Sheria na Katiba zinapasa kutekelezwa kwa njia inayomsaidia mwananchi sio kumuumiza,” akasema kwenye mahojiano na Taifa Leo kwa njia ya simu.

Bw Kigano, ambaye ni Mbunge wa Kangema alisema, suala hilo la usawa wa kijinsia katika mabunge yote mawili limeshughulikiwa kwa undani kwenye ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI) ambayo rasimu yake ya mwisho haijatolewa.

“Isitoshe, kamati yangu ya JLAC imekuwa ikishughulikia suala hili ili kutoa mwelekeo,” akasema.

Kwa mujibu wa kipengele cha 27 (8) cha Katiba, angalau thuluthi moja ya wanaoshikilia nyadhifa za kuchaguliwa na kuteuliwa wanafaa kuwa wa jinsia tofauti.

Lakini wakati huu, kwa mfano, kuna jumla ya Wabunge 72 wa kike kati ya 349 ilhali Katiba inahitaji idadi ya wabunge hao kuwa angalau wabunge 117.

Bunge la kitaifa limejaribu mara nne kupitisha sheria ya kufanikisha hitaji hilo la kikatiba lakini likafeli.

Jaribio la mwisho la Novemba 2019, lilifeli baada ya idadi tosha ya wabunge (angalau 233) kukosa kufikiwa kuwezesha mswada wa sheria hiyo kupigiwa kura.