Maraga asifiwa kwa kuongeza idadi ya korti nchini

Maraga asifiwa kwa kuongeza idadi ya korti nchini

Na SAMMY WAWERU

Utendakazi wa Jaji Mkuu (CJ) David Kenani Maraga na ambaye alistaafu rasmi mnamo Jumatatu, Januari 11, 2021 umesifiwa hasa kwa kusaidia kuongeza idadi ya korti nchini.

Chini ya uongozi wake kama Rais wa Idara ya Mahakama tangu 2016, Bw Maraga amezindua jumla ya korti 22.

Alimrithi mtangulizi wake, Jaji Mkuu Mstaafu, Willy Mutunga.

Korti alizozindua, ujenzi umetajwa kufadhiliwa na Benki Kuu ya Dunia.

CJ Maraga amekuwa akimkosoa Rais Uhuru Kenyatta kwa kutoifadhili idara ya mahakama, akilalamikia mrundiko wa kesi mahakamani kusababishwa na upungufu wa fedha.

Jaji huyo Mkuu ambaye amempokeza rasmi Naibu wake, Bi Philomena Mwilu mamlaka ya uongozi ingawa kwa muda mfupi, pia alisaidia kuongeza idadi ya majaji na mahakimu katika idara ya mahakama.

Hata hivyo, amekuwa akikariri kukerwa na Rais Kenyatta kukataa kuidhinisha majaji 41 waliopigwa msasa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) 2019.

“Katika kipindi changu cha uongozi nimepitia changamoto nyingi, ninawashukuru majaji wenzangu wakiongozwa na naibu wangu kwa kusimama kidete nami,” CJ Maraga akasema kwenye hotuba yake ya mwisho katika hafla fupi ya kustaafu iliyoandaliwa katika Mahakama ya Juu zaidi nchini, jijini Naironi.

Bw Maraga alichukua likizo ya kujiandaa kustaafu mwishoni mwa mwaka uliopita, 2020.

Aidha, alitazamia kustaafu kabla ya kuhitimu umri wa miaka 70.

Kabla kujiunga na Mahakama ya Juu zaidi, alikuwa amehudumu katika mahakama kuu kwa muda wa miaka 18.

CJ Maraga anakumbukwa kwa kuongoza mahakama ya juu zaidi kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa kiti cha urais 2017.

Rais Uhuru Kenyatta na ambaye aliwania kuhifadhi kiti chake, aliapa “kurejelea kutathmini idara ya mahakama”.

Ushindi wake ulifutiliwa mbali baada ya muungano wa Nasa na unaoongozwa na kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuupinga.

Machi 2018 Bw Raila na Rais Kenyatta hata hivyo walizika tofauti zao za kisiasa na kuapa kuunganisha taifa, kufuatia salamu za maridhiano maarufu kama ‘Handisheki’.

You can share this post!

Maraga awataka majaji kusimama kidete akistaafu

Amerika mbioni kumtimua Trump