Habari Mseto

Maraga asikitika mahakama nchini zinatumiwa kama tambara mbovu

May 15th, 2019 2 min read

Na CECIL ODONGO
JAJI Mkuu David Maraga amezitaka Mahakama na mawakili kuheshimu sheria zinazoongoza utendakazi wao ili kurejesha imani ya raia katika korti za hapa nchini.
Bw Maraga alieleza kusikitishwa kwake na jinsi mahakama zimegeuzwa uwanja wa vita vya kisiasa kupitia matamshi ya chuki, propaganda na hadaa tupu kwa umma.
“Inasikitisha jinsi nukuu kwenye katiba hufasiriwa vibaya na mawakili kwa manufaa ya wanasiasa au kwa manufaa ya fedha. Mtindo huu huipa mahakama sura mbaya machoni mwa umma ambao wanazidi kupoteza imani kwenye asasi hii,” akasema Bw Maraga.
Mkuu huyo wa idara ya Mahakama hata hivyo alisikitikia hatua ya mawakili na majaji kupuuza vifungu vya katiba vinavyoongoza utoaji wa maamuzi kwenye kesi mbalimbali.
Bw Maraga alisema hayo wakati wa uzinduzi wa toleo la pili la kitabu kuhusu katiba ya nchi katika Chuo Kikuu cha Strathmore Jumanne jioni.
Kitabu hicho kwa anwani ‘Katiba ya Kenya: Utoaji maoni’ kiliandikwa na Prof PLO Lumumba na Dkt Luis Franceschi. Toleo la kwanza liliandikwa mwaka wa 2014.
Dkt Fraceschi ni Mkuu wa Idara ya kozi ya uanasheria katika Chuo Kikuu cha Strathmore na amekuwa mhadhiri wa masuala ya katiba na sheria za Kimataifa.
Msomi huyo amejivunia sifa sufufu kwa kuchapisha makala mengi na vitabu kuhusu mada mbalimbali yanayohusiana na sheria na maadili.
Prof PLO Lumumba naye ni mlumbi msifika na wakili mashuhuri nchini Kenya. Vile vile, yeye ni wakili katika mahakama kuu nchini Tanzania.
Akipigia debe kitabu hicho, Dkt Franceschi alisema kitawafaa sana mawakili, majaji na wanafunzi wanaosomea kozi za sheria katika vyuo vikuu mbalimbali nchini.
“Kabla ya kuchapisha toleo la kwanza, hakukuwa na mwongozo wowote kuhusu katiba ambao ungetumiwa na wanafunzi wa uanasheria kufanya utafiti wao,” akasema Dkt Franceschi huku akisisitiza kitabu hicho kina hoja za kitaaluma kuhusu katiba.
Baada ya kurasmishwa mwaka wa 2010, katiba mpya imeleta mabadiliko katika mawanda ya kisiasa, kiuchumi na mageuzi mkubwa katika jamii.
“Ili kutimiza lengo lake la kuleta mageuzi, katiba inafaa kusomwa na ibara zote zitekelezwe na kuheshimiwa,” akaongeza Dkt Franceschi.
Kupitia toleo la pili, waandishi wanaonyesha jinsi kila ibara ya katiba inafaa kutekelezwa ili kukithi matamanio ya Wakenya kuishi katika jamii inayozingatia usawa, haki, uongozi bora, maendeleo yasiyobagua na kuheshimu haki za kibinadamu.
Idara ya Mahakama nchini hata hivyo imepiga hatua muhimu katika kuhakikisha katiba inaeleweka na kuitekeleza kikamilifu.