Habari Mseto

Maraga atoka hospitali, mkewe bado atibiwa

December 24th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

JAJI Mkuu David Maraga aliruhusiwa kwenda nyumbani Jumamosi jioni baada ya kuchunguzwa na kutibiwa katika hospitali ya Nairobi.

Jaji Maraga alipelekwa humo baada ya kusafirishwa kutoka hospitali ya War Memorial, Nakuru, alikopelekwa baada ya kupata ajali ya barabarani akiwa na mkewe, Yucabeth, katika eneo la Ngata kwenye barabara ya Nakuru – Eldoret.

Hata hivyo, mkewe bado anaendelea kutibiwa hospitalini humo,” taarifa kutoka hospitali hiyo ilidokeza.

Iliongeza kuwa dereva wao na msaidizi mmoja aliyekuwa ndani ya gari hilo hawakuumia.

Jaji Maraga alipata majeraha madogo licha ya gari lake,aina ya Mercedez Benz kuonekana kuharibika sana baada ya kuhusika katika ajali hiyo.

Alikuwa akielekea kanisani akiwa ameandamana na mkewe na kulingana naye, hiyo ilikuwa ni ajali ndogo, iliyomfanya kubandikwa bendeji usoni.

Katika ujumbe wake kwa wananchi, aliwashukuru kwa kumjulia hali baada ya kuhusika katika ajali hiyo, na pia kumwombea.

“Ninamshukuru sana Rais Uhuru Kenyatta ambaye alitoa agizo ili nisafirishwe hadi Nairobi kwa matibabu zaidi,” alisema.

Alieleza kuwa baada ya uchunguzi wa madaktari, walipatikana walipata majeraha madogo na wamo salama.

Jaji Mkuu alieleza kuwa Bw Kigen, aliyekuwa kwenye gari lingine lililohusika katika ajali hiyo, licha ya kuuguza majeraha makubwa zaidi alikuwa katika hali nzuri.

“Inspekta Mkuu wa Polisi alinihakikishia kuwa Bw Kigen yumo katika hali nzuri. Tunamwombea na tutafanya tuwezacho kumsaidia katika matibabu yake,” alisema katika ujumbe huo na kuwataka wananchi kuwa makini barabarani wanaposafiri kuelekea nyumbani msimu huu wa Krismasi.