Habari MsetoVideo

Maraga awataka majaji na mahakimu wazingatie maadili ili kukuza imani

May 16th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

JAJI Mkuu (CJ) David Maraga Jumatano aliwataka majaji na mahakimu wote wawe na maadili mema ndipo wananchi wawe na imani katika idara ya korti.

Jaji Maraga aliyekuwa anaongoza sherehe ya kumteua Jaji Lydia Achode kuwa Jaji msimamizi wa Mahakama Kuu alisema jukumu kuu la “ maafisa wa idara ya mahakama ni kutekeleza haki pasi kusita.”

“Kile unatakiwa kufanya sasa ni kuimarisha utekelezaji wa huduma ndipo wananchi wa kawaida almaarufu ‘Wanjiku’ wafaidi na huduma za idara ya mahakama,” Jaji Maraga alimshauri Jaji Achode.

Jaji Achode alikuwa anatwaa usimamizi wa mahakama kuu kutoka kwa Jaji Richard Mwongo ambaye alihamishwa kutoka Nairobi.

JAJI Mkuu (CJ) David Maraga awahutubia majaji na mahakimu jijini Nairobi Mei 16, 2018. Picha/ Richard Munguti

Jaji  Achode aliteuliwa mnamo Aprili 23, 2018 katika hafla iliyosimamiwa na maafisa kutoka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Alizoa kura 43 kati ya kura 80 zilizopigwa.

Jaji Achode aliwashinda  wenzake Majaji Mary Kasango na Jaji Asenath Ongeri.

Jaji Achode ambaye ni jaji mwanamke wa kwanza kuteuliwa kuwa msimamizi wa majaji wa mahakama kuu aliajiriwa katika idara ya mahakama kama hakimu.

Alihudumu akiwa hakimu mkazi wa kiwango cha pili (DM2) katika Mahakama ya Kericho mwaka wa 1986.

Jaji Achode ahutubu baada la kulishw akiapo Mei 16, 2018. Picha/ Richard Munguti

Alipandishwa vyeo hadi alipoteuliwa Jaji mwaka wa 2011 na kupelekwa Mombasa.

Kabla ya kuteuliwa Jaji alikuwa anahudumu kwa wadhifa wa Msajili  mkuu wa idara ya mahakama na katibu wa tume ya kuajiri watumishi wa idara ya mahakama.

Mbali na kusimamia majaji wengine na kuhakikisha kuna uangavu katika idara hiyo pia atakuwa mwanachama wa kamati ya kumsahuru Jaji Mkuu (CJ) David Maraga (JLAC).

“Nitahakikisha kuwa sijawakandamiza majaji wenzangu kwa kuwataka mfanye kile mimi siwezi kufanya. Hata mimi ni jaji kama ninyi,” alisema Jaji Achode katika hotuba yake.

Video Gallery