Maraga kustaafu baada ya pandashuka tele akiongoza mahakama

Maraga kustaafu baada ya pandashuka tele akiongoza mahakama

Na RICHARD MUNGUTI

JANUARI 12, 2021, Jaji Mkuu David Kenanu Maraga, atastaafu rasmi baada ya kuhudumu kwa kipindi cha miaka minne baada ya kutimiza umri wa miaka 70. Umri huu ndio majaji wote ustaafu.

Nafasi yake itashikiliwa na naibu wake Jaji Philomena Mbete Mwili, mchakato wa atakayejaza nafasi yake ukianza.

Hata hivyo, Jaji Mwilu amepata vizingiti licha ya Jaji Maraga kumkabidhi mamlaka ya kusimamia idara ya mahakama.Wakati wa kipindi alichohudumu, Jaji Maraga atakumbukwa kuwa Jaji Mkuu mkakamavu ambaye alitekeleza majukumu yake bila kutingisika licha ya dhoruba na mawimbi makali yaliyotishia kuvuruga lengo lake la kuhakikisha Wakenya wote wanapata haki.

Ni Wakenya wachache wanaojua sababu za Jaji Maraga kuwa imara na kusimama kidete kama fito za chuma katika utenda kazi wake.Mbali na kiapo alichokula mbele ya Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi kabla ya kuanza kazi yake rasmi, Jaji Maraga aliongozwa na wakuu wa Kanisa la Seventh Day kuungama kwamba atatenda haki bila woga wala upendeleo ndani ya afisi yake.

Viongozi hao wa Kanisa walimweleza kuwa “Mungu ndiye atakuwa shahidi katika utenda kazi wake wote akiwa na majaji wenzake na akiwa peke yake.”

Kwenye maombi maalum ndani ya afisi yake, Jaji Maraga aliapa mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya viongozi wakuu wa Seventh Day Adventist kwamba “hatashiriki katika ufisadi wa aina yoyote.”

Alipokuwa akihojiwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC), Jaji Maraga aliungama “atatosheka na mshahara atakaokuwa anapokea kutokana na utendakazi wake akiwa Jaji Mkuu wa Kenya na Rais wa Mahakama ya Juu.”

Maungamo haya ya Jaji Maraga aliyasema huku amepiga magoti ndani ya afisi yake katika hafla iliyoshuhudiwa na mwanahabari huyu wetu Richard Munguti mnamo Oktoba 19, 2016.

Jaji Maraga alifahamishwa na wakuu hao wa makanisa ya Seventh Day Adventist kuwa afisi yake “itakuwa madhabahu ya utendaji haki na usawa kwa Wakenya wote bila upendeleo.”

Jaji Maraga alielezwa kinaga ubaga na viongozi hao wa kidini kwamba “kuna athari za kutenda kinyume cha maungamo yake na kiapo chake cha kutenda haki kwa wote bila upendeleo kwa mujibu wa sheria za Mungu, Katiba na Sheria zinazothibiti nchi hii.”

Mizani ya kupima utiifu wa Jaji Maraga kwa viapo na maungamo yake ulikuwa ni uchaguzi mkuu wa 2017 ambapo yeye, naibu wake Jaji Philomena Mbete Mwilu, Jaji Smokin Wanjala na Jaji Isaac Lenaola walifutilia mbali ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta.

Majaji Jackton Ojwang na Njoki Ndung’u walitofautiana na uamuzi wao kuwa “uchaguzi huo mkuu wa 2017 haukuendelezwa kwa mujibu wa sheria na kuufutilia mbali.”

Wakati huo Jaji Mohammed Ibrahim hakuwa nchini alikuwa amepelekwa ng’ambo kwa matibabu maalum baada ya kuugua kesi hiyo ikiendelea.

Katika uamuzi huo Jaji Maraga na majaji wenzake walisema “uchaguzi huo uliborongwa na kuvurugwa kumfaidi Rais Kenyatta.”Mlalamishi katika kesi hiyo alikuwa ni Raila Odinga wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) na naibu wake Kalonzo Musyoka wa Chama cha Wiper Democratic Party (Wiper).

Kwenye kesi hiyo Bw Odinga alidai mitambo ya kieletroniki iliborongwa na kuvurugwa ndipo matokeo ya uchaguzi yamfaidi Rais Kenyatta aliyetangazwa ameshinda uchaguzi huo kwa asilimia 54 naye Bw Odinga akiwa wa pili kwa kuzoa kura kwa asilimia 44.

Tofauti ya kura kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga ilikuwa kura 1.4milioni.Kabla ya uchaguzi huo kufanyika afisa mkuu katika tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) aliyekuwa anasimamia kitengo cha ICT, Chris Musando aliuawa katika hali tatanishi.

Baada ya kufutilia mbali uchaguzi huo Jaji Maraga aliingia katika kumbukumbu za historia kuwa Jaji Mkuu wa kwanza nchini na ulimwenguni kufutilia mbali ushindi wa rais kwenye uchaguzi mkuu.

Uamuzi huu uliletea idara ya Mahakama sifa sufufu na wanasiasa wakawa kitako wakijua chochote kinaweza kuwatendekea wakikaidi sheria.Baada ya uamuzi huo wa Jaji Maraga Rais Kenyatta alisema “ atarejelea suala la idara ya mahakama.”

Katika mchakato wa mageuzi ya katiba kuna pendekezo idara ya mahakama isimamiwe na afisa atakayekuwa anapokea malalamishi kuwahusu majaji.

Uamuzi huo wa 2017 ulitia chachu uhusiano wa Rais Kenyatta na Jaji Maraga hata ikachangia kutoapishwa kwa majaji 41 wa mahakama ya rufaa na mahakama kuu na Rais.

Pia bajeti ya idara ya mahakama ilipunguzwa kutoka Sh2.1bilioni hadi Sh50 milioni.

Jaji Maraga ataondoka na kuacha uhusiano kati yake na Rais Kenyatta ukiwa umekinzana lakini amedumisha msimamo wake wa kutetea haki na uhuru wa idara ya mahakama.

Jaji Maraga amesema ijapokuwa amepokea vitisho katika utendakazi wake atastaafu na kuishi kwa amani Kaunti ya Nakuru ambapo alijitafutia shamba alipokuwa akihudumu kama wakili.

You can share this post!

Matiang’i apotosha kuhusu uhalifu

Wabunge wataka CDF iongezwe kujenga madarasa