Habari Mseto

Maraga, Matiang'i na Haji kukutana kujadili mageuzi katika kesi za ufisadi

November 13th, 2019 1 min read

Na BENSON MATHEKA

JAJI Mkuu David Maraga, Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP0, Noordin Haji watakutana na wakuu wa idara zinazohusika na haki kwenye kongamano la kutathmini mageuzi katika mfumo wa utoaji haki katika kesi za uhalifu.

Mkutano huo wa kwanza nchini utafanyika wakati ambapo Bw Maraga amelalamika vikali kwamba idara yake inadunishwa na kulemazwa kwa kunyimwa pesa huku serikali ikiilaumu kwa kuwa kizingiti katika vita dhidi ya ufisadi.

Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai Bw George Kinoti, Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi Twalib Mbarak na Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai, watahudhuria kongamano hilo la siku mbili katika mkahawa wa Great Rift Valley Lodge mjini Naivasha.

Ilani iliyochapishwa katika tovuti ya Mahakama ilisema kwamba Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki na Kamishna wa Magereza Wycliffe Ogalo pia watahudhuria mkutano huo.

Mkutano huo unafanyika wiki moja baada ya Bw Maraga kukemea serikali kwa kutaka kuingilia uhuru wa mahakama naye Rais Uhuru Kenyatta akimlaumu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake.

Mfumo mbadala

Bw Haji majuzi alizindua mfumo mbadala wa kutatua kesi za ufisadi akilenga kupunguza muda ambao kesi hizo huchukua kortini.

Katika mfumo huo, washtakiwa hujadiliana na ofisi yake wakubali mashtaka na kurudisha pesa wanazokubali kuiba ili wapunguziwe adhabu.

Bw Maraga amekuwa akitetea mahakama dhidi ya lawama kwamba inalemaza vita dhidi ya ufisadi kwa kuwapa washukiwa dhamana nafuu na kutoa maagizo yakisitisha uchunguzi wa kesi hizo.

Amekuwa akilaumu ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka na idara ya upelelezi kwa kutowasilisha ushahidi wa kutosha.

Katika kongamano hilo wakuu hao wanatarajiwa kujadili mageuzi yanayofaa ili kuhakikisha kesi zinasikilizwa na kuamuliwa kwa muda mfupi.