HabariSiasa

Maraga: Najua Wakenya wamechoka lakini nina imani Uhuru atazima ufisadi

May 26th, 2018 1 min read

BERNARDINE MUTANU na CHRIS WAMALWA 

JAJI Mkuu David Maraga (pichani) amewataka Wakenya wanaoishi nje ya nchi kutotamaushwa na Kenya licha ya ufisadi mwingi unaoshuhudiwa nchini.

Akiongea wakati wa kuzindua mkutano wa wananchi wanaoishi nje ya nchi mjini Dallas, Texas, Ijumaa, Jaji Maraga alisema alijua kuwa Wakenya wengi nje ya nchi wameghadhabishwa na ripoti za ufisadi nchini.

“Rais Uhuru Kenyatta amehakikishia Wakenya kwamba serikali yake itakabiliana na wahusika katika visa hivyo. Na ndio maana ninawaomba kutotamaushwa na taifa lenu. Huu ndio wakati wa kuwa wazalendo,” alisema Jaji Maraga.

Alisema kutokana na ripoti hizo, alielewa kuwa Wakenya wamechoka lakini pia akaeleza kuwa serikali ilikuwa tayari kukabiliana na ufisadi katika taasisi za umma.

“Ninajua changamoto zinazokabiliwa nchini zinaweza kuwafanya wengi kufikiria kuwa Kenya imeanguka na hakuna tumaini tena. Lakini Kenya inaendelea na kuna matumaini,” alisema Jaji Maraga.

Bw Maraga alisema Mahakama imezindua mikakati ya kukabiliana na ufisadi na itaendelea kupigana na uovu huo.

“Kuhukumiwa kwa maafisa wakuu wa Kaunti ya Nairobi ni ishara wazi kwamba tumejitolea kukabiliana na changamoto hiyo.

Demokrasia yetu inaweza kuwa tete, lakini inakua na kuimarika. Taasisi zetu zinaweza kuwa changa, lakini zimejaribiwa na bado zipo,” alisema Bw Maraga.