Michezo

Marathon ya Olimpiki Tokyo kuanza alfajiri

April 18th, 2019 2 min read

Na MWANDISHI WETU

MAKALA ya 32 ya Michezo ya Olimpiki itakayoandaliwa jijini Tokyo, Japan mwakani yatafungwa rasmi kwa mbio za marathon kwa upande wa wanaume mnamo Agosti 9.

Haya ni kwa mujibu wa ratiba ya michezo hiyo ambayo imepangiwa kufunguliwa kwa matembezi ya kilomita 20 kwa upande wa wanaume mnamo Ijumaa ya Julai 31, 2020 katika ukumbi wa Tokyo Imperial Palace.

Kati ya Julai 31 na Agosti 9, michezo 17 itaandaliwa katika uga wa Tokyo Olympic.

“Ratiba ya Olimpiki za Tokyo 2020 ni tofauti sana na jinsi ambavyo michezo hiyo imekuwa ikiendeshwa hapo awali. Hata hivyo, mashabiki watakuwa na fursa nzuri za kushuhudia hafla zote za kutolewa kwa medali mbalimbali. Kati ya fainali 17 za michezo mbalimbali, 15 zitafanyika katika uwanja mkuu wa Tokyo Olympic,” akasema Mkurugenzi wa Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF), Paul Hardy.

Kwa mujibu wa vinara wa michezo hiyo, nyingi za fainali zitaandaliwa wakati wa majira ya asubuhi kama ilivyoagizwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC).

Ombi la IOC lilitolewa mahsusi kwa lengo la kuwaepusha wanariadha na mashabiki na joto jingi linalotarajiwa jijini Tokyo wakati wa mashindano hayo.

Ingawa hivyo, baadhi ya fani za michezo mbalimbali zitafanyika nyakati za jioni baada ya jua kutua. Kulingana na waratibu, michezo hii ni pamoja na mbio za masafa mafupi nay a kadri.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya michezo hiyo, Olimpiki za Tokyo zitashuhudia mbio za kupokezana vijiti za 4×400 kwa upande wa wanaume na wanawake zikiandaliwa sambamba.

Fainali za fani tisa zimepangiwa kufanyika wakati wa majira ya asubuhi. Fani hizi ni pamoja na marathon zote za upande wa wanaume na wanawake pamoja na fainali.

Kwa mujibu wa ratiba, fainali za mbio za mita 100 na mita 200, mita 200 na mita 400, mita 800 na mita 1500, mita 1500 na mita 5000, mita 5000 na mita 10,000 zimepangwa kwa namna itakayoruhusu wanariadha walio na uwezo wa kushiriki zaidi ya fani moja kufanikisha maazimio yao.

Wanariadha kutoka Kenya, wakiwemo bingwa wa dunia Eliud Kipchoge na mwenzake Mary Keitany, wanatazamiwa kutamba zaidi katika Marathon sawa na Wakenya wengine katika fani mbalimbali za mbio za masafa ya kadri hasa mita 800, mita 3000 kuruka maji na viunzi, mita 5000 na mita 10,000.

Masafa marefu

Mbio zote za masafa marefu na kadri zimepangiwa kuanza mapema ya saa kumi na mbili alfajiri huku matembezi ya kilomita 50 kwa upande wa wanaume yakianza mnamo saa kumi na moja alfajiri.

Kitengo cha kwanza kabisa cha Michezo ya Olimpiki ni matembezi ya kilomita 20 ambapo wenyeji Japan wanapigiwa upatu kushiriki kwa wingi na kuweka hai matumaini ya kutwaa nishani za dhahabu, fedha na shaba.

Kitengo cha decatholon na heptathlon kitaandaliwa kwa siku mbili tofauti (Agosti 5 na 6) ili kutoa fursa kwa mashabiki kufurahia zaidi mashindano hayo.

Ratiba pia inawapa nafasi wanariadha watakaoshiriki mbio za mita 400 kushiriki fani ya mbio za kupokezana vijiti vya 4×400. Mbio hizo zitaandaliwa pia kwa siku mbili.