HabariHabari Mseto

Marehemu arejeshwa mochari kwa kukosa pa kuzikwa

February 12th, 2018 2 min read

Na MOHAMED AHMED na BRIAN OCHARO

Kwa Muhtasari:

  • Familia ilikuwa imechimba kaburi na kukamilisha mipango ya mazishi wakati iliarifiwa na askari wawili kusitisha mipango hiyo
  • Yasema mwenye shamba aliwasilisha kesi kortini kutaka mipango yote ya mazishi isitishwe 
  • Mlalamishi asema kuwa atapoteza shamba lake iwapo mwili huo utazikwa katika ardhi yake
  • Familia ya mwendazake sasa inaomba Mahakama ya Juu kuingilia kati na kuwapa ruhusa kuzika mtoto wao

KABURI la mwanamume wa umri wa miaka 43 Bw Edward Mwambui litabakia wazi katika shamba lao lililoko Kiembeni, Mombasa kutokana na mvutano kuhusu umiliki wa ardhi.

Bw Mwambui, ambaye amekuwa akifanya kazi katika Halmashauri ya Bandari nchini (KPA), hana amani wiki moja baada ya kuugua na kufa kutokana na kaburi lake kuchimbwa katika shamba la wenyewe.

“Alifariki siku ya Jumapili wiki iliyopita baada ya kuugua ugonjwa wa homa ya mapafu. Tulikuwa tumechimba kaburi na kukamilisha mipango ya mazishi wakati tuliarifiwa na askari wawili kusitisha mipango hiyo,” Bi Josephine Hongo, ambaye ni dadaye mwendazake alisema.

Siku ya Ijumaa, familia ya mwendazake ilikuwa imesafirisha mwili wake kutoka hospitali kuu ya kanda ya eneo la Pwani tayari kumzika katika shamba hilo kulingana na mapenzi yake lakini safari hiyo ilisitishwa ghafla kwa sababu ya mzozo huo.

 

Agizo la korti

“Tulikuwa tunaupeleka mwili katika kanisa la Jesus Power kwa maombi kabla ya kumpeleka nyumbani kuzikwa. Tulikutana na maafisa wawili ambao walitupa nakala ya kortini ambayo ilitueleza turejeshe mwili katika chumba cha kuhifadhi maiti hadi mgororo kuhusiana na shamba hilo utatuliwe,” alisema.

Wakiongea na Taifa Leo nyumbani kwake Kashani, Kiembeni, familia ya mwendazake ilisema mwenye shamba hilo aliwasilisha kesi kortini kutaka mipango yote ya mazishi isitishwe  kutokana na tofauti kuhusu umiliki wa shamba.

“Kaka yangu alinunua hilo shamba kwa Sh1.7 millioni mwaka wa  2014 kutoka kwa mlalamishi ambaye amewasilisha kesi kortnini kusitisha mazishi. Mwendazake tayari alikuwa amelipa Sh1 millioni na walikubaliana kulipa pesa zilizosalia baada ya kupata hati ya kumiliki ardhi hiyo,” alisema.

Nakala ya mashitaka ambayo ilipatiwa mamake mwendazeke Bi Ms Prisca Kavua inamzuia kumzika mwanawe katika ardhi hiyo kwasababu  hilo shamba si lake.

 

Atapoteza shamba

Bi Josephine Tole ambaye aliwasilisha kesi hiyo katika mahakama ya Mombasa anasema kuwa atapoteza shamba lake iwapo mwili huo utazikwa katika ardhi yake .

“Kama koti  haitapeana amri kutokana na ombi la mlalamishi(Bi Tole), mlalamishi atapata hasara kwani shamba lake litakuwa na kaburi la mtu ambaye hana uhusiano na  faida kwa familia yake,” Bi Tole alisema katika nakala hiyo ambayo iliwasilishwa mahakamani na Ndegwa Katisya Advocates.

Mshtakiwa pia analaumiwa kwa kupanga kuzika mwili wa motto wake katika shamba hilo licha ya kufahamu kuwa yeye siyo mmiliki wa ardhi hiyo.

Familia ya mwendazake sasa wanaomba mahakama ya juu kuingilia kati na kuwapa ruhusa kuzika mtoto wao huku wakiendelea na kesi kotini.

Bi Hongo alisema ndugu yake ambaye alikuwa ameajiriwa katika bandari hiyo aliwaacha watoto wanne na mjane.
Mwili wa mwendazake uliregeshwa katika chumba cha kuhifadhi maiti huku kesi hiyo ikiendelea.