Bambika

Marehemu Chongin Kale kukumbukwa kwa kuigiza jenezani

March 21st, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

MCHESHI Nicholas Rotich almaarufu Chongin Kale aliyefahamika vyema kupitia mzaha wake akilala ndani ya jeneza, alithibitishwa kwamba aliaga dunia katika ajali mbaya ya barabarani iliyofanyika Machi 18, 2024, katika Kaunti ya Bomet.

Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Silibwet kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Bomet ya Kati Bw Musa Imamai.

Jumla ya watu watano walifariki huku wengine 18 wakipata majeraha ya viwango mbalimbali.

Chongin Kale alikuwa mmojawapo wa hao watano waliopoteza maisha yao.

“Familia ya msanii huyo ilitambua mwili wake,” akasema Bw Imamai.

Kifo cha mcheshi huyo kilijiri saa chache baada ya kutuma risala zake za rambirambi kufuatia mauti ya ‘tiktoker’ Brian Chira aliyeaga mnamo Machi 16, 2024, katika Kaunti ya Kiambu baada ya kugongwa na gari.

Katika risala zake kwa mwendazake, Chongin kupitia ukurasa wake wa Facebook alikuwa ameandika kwamba ni uchungu kumpoteza Bw Chira katika umri wake mdogo.

“Lala salama ndugu yangu,” akasema.

Chini ya siku mbili baadaye naye akamfuata Chira.

Kwa mujibu wa Bw Imamai, Chongin alikuwa akisafiria gari aina ya matatu akielekea mjini Bomet.

“Gari hilo lilitoka kwa mkondo wake na likagongana ana kwa ana na trekta, hali ambayo ilisababisha maafa hayo,” akasema Bw Imamai.