Habari MsetoSiasa

Marekebisho katika BBI yaja – Wanasiasa

December 1st, 2019 2 min read

Na JUSTUS OCHIENG’

MJADALA kuhusu ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) Jumapili uliendelea kuchacha, wandani wa Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa Upinzani Raila Odinga wakiwahakikishia Wakenya kwamba masuala ibuka ambayo hayakujumuishwa yatawasilishwa kwa kamati ya wataalamu kwenye stakabadhi ya mwisho itakayopigiwa kura ya maoni.

Matamashi ya wanasiasa wanaorindimisha ngoma ya wawili hao yanajiri huku baadhi ya Wakenya wakilalamika kwamba ripoti hiyo haikuangazia mambo muhimu yatakayochangia kufanikiwa kwa umoja wa taifa.

Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna, mwenzake wa Jubilee Raphael Tuju, Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata, Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru, Katibu Mkuu wa Cotu, Mbunge wa Kisumu Mashariki Shakeel Shabbir na mwenzake wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu ni kati ya viongozi waliounga mkono BBI na kutoa wito kwa marekebisho kufanyiwa ripoti ya mwisho kabla ya kuandiliwa kwa kura ya maoni.

Bw Sifuna aliwataka Wakenya kutokuwa na wasiwasi kuhusu BBI akiahidi kwamba masuala ambayo yaliachwa nje yatajumuishwa na kamati ya waatalamu.

“Mjadala umeanza na tutakuwa na nafasi ya kusanifisha na kujumuisha mapendekezo yote katika ripoti ya mwisho,” Bw Sifuna alisema.

Bw Tuju naye Ijumaa wiki jana wakati wa mahojiano katika idhaa ya Mayienga FM inayopeperusha matangazo kwa lugha ya Kiluo alisema baadhi ya hoja nzito kwenye BBI zinazua mdahalo na lazima zirekebishwe ili kuwaridhisha Wakenya.

“Ripoti ya BBI ni sauti ya raia na hatua inayofuatia ni kuikabidhi kwa kamati ya wataalamu ili kuiangazia na kutatua mambo yote yanayoibuliwa,” akasema Bw Tuju.

“Kwa mfano pendekezo kwamba Waziri Mkuu atakuwa akilipwa mshahara kama mbunge pekee ni hatari na huenda Likasababisha ajihusishe na ufisadi ili kupata fedha zaidi,” akaongeza.

Mbunge huyo wa zamani wa Rarieda, hata hivyo aliashiria kwamba anaunga mkono pendekezo la BBI kufikishiwa raia kupitia kura ya maamuzi badala ya kupitia bunge.

Bw Atwoli ambaye ameonekana kutoridhishwa na BBI naye alisema kwamba nafasi mbili za manaibu wa waziri mkuu na manaibu wawili wa rais zinafaa kubuniwa huku akisisitiza waziri mkuu aongezewe mamlaka kuliko jinsi ilivyo kwenye BBI iliyozinduliwa wiki jana.

Mtetezi huyo wa wafanyakazi alisema taifa hili linafaa likumbatie mfumo wa utawala wa bunge akisisitiza kuwa viongozi wa upinzani pia wanafaa kupewa nafasi serikalini baada ya uchaguzi.

“Ikiwa tutaendelea kukwamilia mfumo wa sasa unaompa rais mamlaka makubwa na tusikumbatie utawala wa ubunge basi Wakenya wataendelea kupigana. Wanaowasilisha maoni kwa kamati ya wataalamu wanafaa kujumuisha hoja hiyo,” akasema Bw Atwoli.

Kwa upande wake, Bw Kang’ata hata hivyo alisema kwamba mapendekezo ya sasa kuhusu wadhifa wa waziri mkuu hayafai kufanyiwa marekebisho akisema atakuwa akiunganisha bunge na afisi ya Rais.