Habari

Mariga atetemesha ODM, Kieleweke

August 30th, 2019 2 min read

Na JUSTUS OCHIENG na CECIL ODONGO

UWEZEKANO wa kuteuliwa kwa mwanasoka McDonald Mariga kuwania kiti cha ubunge cha Kibra umetetemesha chama cha ODM na mrengo wa Kieleweke wa chama cha Jubilee.

Bw Mariga, ambaye aliacha kuichezea Harambee Stars miaka kadhaa iliyopita, ameitwa ‘kutoka benchi’ na mrengo wa ‘Tangatanga’ unaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto ili kuusaidia ‘kushinda kombe’ katika uchaguzi mdogo wa Novemba 7.

Duru za kuaminika ndani ya Jubilee ziliambia Taifa Leo kwamba Dkt Ruto anashinikiza Bw Mariga ateuliwe kupeperusha tiketi ya Jubilee kwa matumaini kuwa ataweza kuzoa kura za jamii ya Waluhya na vijana katika eneo bunge hilo lililo na wapiga kura wengi wenye sifa hizo mbili.

Lakini kwa upande mwingine, upande wa Kieleweke ambao unaegemea mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta kwenye Jubilee, hautaki Bw Mariga apate tiketi hiyo kwa hofu kuwa atakuwa tisho kwa mgombeaji wa ODM.

Hii inatokana na kuwa mrengo wa Kieleweke hauko makini Jubilee kushinda kiti hicho kutokana na handisheki kati ya Rais Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga.

“Mrengo wa Kieleweke unataka mwaniaji asiyekuwa na ufuasi mkubwa wala pesa za kutetemesha katika kampeni, kama njia ya kuendeleza urafiki uliotokana na handisheki,” akasema afisa wa ngazi ya juu Jubilee.

Akiungwa mkono na Dkt Ruto, Bw Mariga atakuwa na uwezo wa kufanya kampeni inayoweza kuvuruga mpango wa ODM kwenye uchaguzi huo.

Uwezekano wa kuwepo kwa Bw Mariga kwenye kinyang’anyiro hicho ulitajwa jana kama moja ya sababu za ODM kuahirisha mchujo wake uliokuwa umepangwa kufanyika kesho. Sasa uteuzi huo utafanywa Septemba 7 ili kukipa muda wa kuona iwapo Bw Mariga atakuwa debeni kabla ya kuteua mwaniaji wao.

Mvutano

Mvutano ndani ya Jubilee kuhusu mwanasoka huyo aliyecheza kimataifa Italia na Uhispania, pia ulitajwa kuwa sababu ya chama cha Jubilee kukosa kutangaza orodha ya watu tisa ambao kilisema tayari wamewasilisha maombi ya kupewa tiketi ya kuwania ubunge Kibra.

“Upande wa Kieleweke hautaki Bw Mariga. Mrengo wa Dkt Ruto nao unasisitiza ndiye unataka,” zikasema duru za Jubilee.

Chama cha Amani National Congress nacho kinatumia mbinu hiyo hiyo ya kutegemea kura nyingi za Waluhya kwa kumwidhinisha Eliud Owalo apeperushe bendera yake.

Bw Owalo si mgeni Kibra kwani alivurugana na bintiye kinara wa chama cha ODM, Bi Rosemary Odinga kwenye mchujo wa kuwania kiti hicho 2017.

Akizungumza aipozinduliwa rasmi mnamo Jumatano, Bw Owalo alisikitika kuwa wakazi wa eneobunge hilo wamejawa na umaskini mwingi miaka 56 tangu Kenya ijinyakulie uhuru.

“Nimebainisha kwamba tatizo kuu ni namna matatizo yanayowakabili watu wa Kibra yanavyotatuliwa na pia umaskini katika taifa lote. Nina uwezo na mbinu za kubadili mambo,” akasema Bw Owalo.

Huku upande wa ‘Tangatanga’ ukiendelea kumpigia debe Bw Mariga, duru zinaarifu kwamba jamii ya Waluhya walioko ODM inamuunga mkono kiongozi wa vijana Benson Musungu.

Kwa upande wao, Waluo wanamuunga mkono mwalimu mkuu wa Shule ya Dagoretti, Bw Peter Orero.

Jambo hili linamfanya Bw Odinga ajikune kichwa zaidi kuhusu mwaniaji atakayeshinda mchujo na kupata tiketi ya chama.