Mario Gotze kuagana rasmi na Dortmund mwishoni mwa msimu huu

Mario Gotze kuagana rasmi na Dortmund mwishoni mwa msimu huu

Na CHRIS ADUNGO

NYOTA wa timu ya taifa ya Ujerumani, Mario Gotze, atavunja rasmi ndoa kati yake na Borussia Dortmund mwishoni mwa msimu huu wa 2019-20.

Haya ni kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Spoti kambini mwa Dortmund, Michael Zorc, ambaye amefichua kwamba fowadi huyo anahemewa na klabu kadhaa maarufu za bara Ulaya zikiwemo Leicester City, Liverpool, Bayer Leverkusen na AC Milan.

Hadi kufikia sasa, Gotze, 27, amewajibishwa na Dortmund katika jumla ya mechi 201 japo amepangwa katika kikosi cha kwanza cha klabu hiyo katika jumla ya michuano mitano pekee ya Bundesliga msimu huu.

Sogora huyo wa zamani wa Bayern Munich anajivunia ufanisi wa kunyanyua ubingwa wa taji la Bundesliga mara tano na ndiye aliyeafungia Ujerumani bao la ushindi dhidi ya Argentina na kuwanyakulia ufalme wa Kombe la Dunia mnamo 2014 nchini Brazil.

“Tutakatiza uhusiano na Gotze mwishoni mwa msimu huu. Mwenyewe atabainisha atakakopania kuelekea hapo baadaye. Maagano yetu naye yatafanikishwa kwa mpangilio mzuri kwa kuwa tumeyaheshimu sana maamuzi yake. Ni miongoni mwa wanasoka wa haiba kubwa watakaofanya vyema katika kikosi chochote duniani,” akasema Zorc.

Tangazo la Zorc linatolewa siku chache tu baada ya kocha Lucien Favre wa Dortmund kusisitiza kwamba mfumo wa mchezo anaotaka waajiri wake kukumbatia unamweka katika ulazima wa kutohitaji tena huduma za Gotze aliyepangwa kwenye benchi la wachezaji wa akiba katika ushindi wa 2-0 uliosajiliwa na Dortmund dhidi ya Wolfsburg katika Bundesliga mnamo Mei 23, 2020.

“Gotze amekuwa akipata nafasi katika kikosi cha kwanza kila tunapotumia mfumo wa 4-4-2. Kwa sasa tunalenga kukumbatia mfumo wa 3-4-3 ambao sidhani utampa fursa nyingi za kutuchezea tena. Nimezungumza naye na tumeafikiana kwamba mfumo huo hautamfaidi sana,” akasema Favre.

You can share this post!

Sita wafa katika ajali

Klabu za La Liga zataka soka ya Uhispania irejelewe Juni 8...

adminleo