Makala

MARTHA NJOROGE: Mola anisaidie nimfikie Rita Dominic

March 22nd, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

PENYE nia pana njia. Ndiyo ameanza kupiga ngoma lakini anaamini uigizaji ni ajira inayoweza kusaidia kizazi kipya hapa nchini.

Martha Karira Njoroge ni kati ya waigizaji wanaoibukia wanaopania kutinga upeo wa kimataifa miaka ijayo.

Katika mpango mzima anasema: “Nimegundua ninacho kipaji katika uigizaji ndiyo maana mwaka uliypita niliamua kuanza kushiriki masuala ya maigizo.”

Ingawa hajafanikiwa kupiga hatua kubwa katika sekta hii anasema tangu akiwa mtoto alitamani kuhitimu kuwa mwanasaikolojia.

”Bila shaka ninaamini nina uwezo tosha kufanya filamu za Kiswahili na lugha zingine kufikia upeo wa kimataifa,” alisema na kuongeza kuwa hata hivyo shangamoto kubwa ni kupata nafasi ya kuigiza maana bado hajakomaa katika tasnia hiyo.

Dada huyu anasema angependa zaidi kushiriki filamu za Kinigeria (Nollywood). Anadokeza kuwa huvutiwa zaidi na mwigizaji mahiri nchini humo kwa jina Rita Dominic. Msanii huyo anajivunia kutwaa tuzo nyingi tu katika uigizaji.

Kwenye shindano la ‘Africa Movie Academy mwaka 2012 alinasa tuzo ya mwigizaji bora Best actress in leading role’. Kadhalika Rita anajivunia kushiriki filamu kocho kocho ikiwamo ‘Finding mercy,’ ‘White waters,’ ‘The Meeting’ na ‘Iyore’ kati ya zingine.

Aidha anasema huvutiwa zaidi na kazi yake mwigizaji wa kimataifa, Nikolina Kamenova Dobreva maarufu kama Nina Dobrev mzawa wa Canada. Ni msanii na mwana mitindo anayejivunia kuigiza filamu nyingi tu ikiwamo ‘The Vampire Diaries,’ ‘Return of Xander,’ ‘ Fam,’ na ‘Lets be Cops,’ kati ya zinginezo.

Hapa Kenya angependa sana kufikia hadhi ya mwigizaji na produsa, Naomi Kamau ambaye katika ushiriki wake hujituma mithili ya mchwa.

Martha mwenye umri wa 21 anajivunia kushiriki filamu moja iitwayo ‘Maciaro ma mwitio,’ iliyozalishwa na Heartmedia Services.

Anasema filamu hiyo inatazamiwa kupeperushwa kupitia runinga ya Mt Kenya. ”Kusema kweli endapo filamu hiyo itapata mpenyo na kuonyeshwa nina imani itanifungulia milango yangu katika masuala ya maigizo,” alisema.

Dada huyu anatoa mwito kwa serikali angalau isaidie sekta ya filamu maana imefurika vijana wengi waliotunukiwa talanta ya uigizaji.

Ingawa anasema sekta ya uigizaji ina changamoto nyingi anashauri wenzie nyakati zote kuwa wavumilivu bila kutarajia utajiri wa haraka.

Pia anawashauri kuwa watie bidii kwenye jitihada za kukuza talanta zao bila kuweka katika kaburi la sahau kujikumbali kwa maumbile yao. Kadhalika anawahimiza kuwa wasisahau kumtegemea Mungu kwa kila jambo wanalofanya.

”Katika mtazamo wangu itakuwa muhimu kwa maprodusa kuwapa wasanii chipukizi nafasi ili kuonyesha talanta zao,” alisema na kuongeza kuwa waliowatangulia hawana budi kuwaonyesha wanaokuja mwongozo mwema katika tasnia ya maigizo.