Michezo

Martial aipa United 'hat trick' ya kwanza tangu Fergie aondoke

June 25th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

ANTHONY Martial alifunga jumla ya mabao matatu na kusaidia waajiri wake Manchester United kuwapepeta Sheffiled United 3-0 katika gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Juni 24 uwanjani Old Trafford.

Ilikuwa ni mara ya kwanza baada ya kipindi cha miaka saba kwa Man-United kufunga jumla ya mabao matatu katika mechi moja, ‘hat-trick’.

Robin van Persie ndiye mchezaji wa mwisho kufungia Man-United hat-trick katika kipute cha EPL na kusaidia kikosi hicho kutawazwa mabingwa mara 13 wa soka ya Uingereza chini ya aliyekua mkufunzi Sir Alex Ferguson.

Bao la kwanza la Martial lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na chipukizi Marcus Rashford kunako dakika ya saba. Fowadi huyo mzawa wa Ufaransa alipachika wavuni mabao mengine katika dakika ya 44 na 74 baada ya kumegemewa pasi mbili murua kutoka kwa Bruno Fernandes.

Matokeo hayo yaliwapaisha Man-United hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali kwa alama 49, mbili pekee nyuma ya Chelsea wanaofunga orodha ya nne-bora. Chelsea walitarajiwa kuwa wenyeji wa mabingwa watetezi Manchester City uwanjani Stamford Bridge mnamo Juni 25.

Chini ya kocha Chris Wilder, Sheffield United kwa sasa wamejizolea alama moja pekee kutokana na mechi tatu zilizopita tangu kurejelewa kwa soka ya EPL iliyokuwa imesitishwa kwa sababu ya janga la corona kuanzia Machi 13, 2020.

Ubora wa matokeo yaliyodhihirishwa na Martial kwa ushirikiano na Fernandes na Rashford, ulimwondolea kocha Ole Gunnar Solskjaer presha na lawama alizokuwa akielekezewa kwa maamuzi ya kuzinadi huduma za Romelu Lukaku na kumtuma mfumaji Alexis Sanchez hadi Inter Milan kwa mkopo mwanzoni mwa msimu huu.

Katika jumla ya mechi saba za EPL ambazo Fernandes aliyesajiliwa kutoka Sporting Lisbon ya Ureno kwa kima cha Sh6.5 bilioni amewajibishwa na Man-United, Martial amepachika wavuni mabao sita.

Nyota huyo kwa sasa anajivunia magoli 19 kutokana na mapambano yote ya msimu huu akivalia jezi za Man-United. Martial anapigiwa upatu wa kuvunja rekodi ya Laukaku aliyefungia Man-United jumla ya mabao 27 katika kipindi cha misimu miwili iliyopita.

Ingawa hivyo, mfumaji Sergio Aguero wa Man-City anajivunia kufunga hat-trick 11 katika kipindi ambapo Man-United wamewezesha kujizolea mbili pekee.

Man-United kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Norwich City katika raundi ya sita ya Kombe la FA mnamo Juni 27 huku Sheffield United wakiwa wenyeji wa Arsenal siku moja baadaye uwanjani Bramall Lane.