Martial asema huu ndio wakati mwafaka zaidi kwake kuondoka Man-United

Martial asema huu ndio wakati mwafaka zaidi kwake kuondoka Man-United

Na MASHIRIKA

FOWADI Anthony Martial, 26, amewataka Manchester United kumwachilia atafute hifadhi mpya mnamo Januari 2022.

Kocha mshikilizi wa Man-United, Ralf Rangnick amesema amelizungumza na Martial kwa muda mrefu mnamo Jumatano usiku wiki jana na sogora huyo raia wa Ufaransa akamweleza kuwa “huu ndio wakati bora zaidi kwake kuruhusu mabadiliko kutokea katika safari yake ya kitaaluma.”

Hadi kufikia sasa, Martial amepangwa katika kikosi cha kwanza cha Man-United mara mbili pekee kutokana na mechi 16 za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na akafunga bao moja.

Licha ya Martial kusisitiza haja ya kuondoka uwanjani Old Trafford, Rangnick amethibitisha kwamba Man-United hawajapokea ofa yoyote kutoka kwa kikosi chochote kinachohemea maarifa ya mshambuliaji huyo wa zamani wa AS Monaco.

Mwanzoni mwa Disemba 2021, Philippe Lamboley ambaye ni wakala wa Martial alifichua kwamba mteja wake alitaka kuagana rasmi na Man-United mnamo Januari 2022 na akaongeza kuwa “angezungumza na Man-United haraka iwezekanavyo kuhusiana na mpango wa sogora huyo.”

Kwa upande wake, Rangnick alisema: “Martial aliniambia amekuwa Man-United kwa miaka saba iliyopita na sasa anahisi huu ndio wakati mwafaka wa kuyoyomea kwingineko kukabiliana na changamoto mpya.”

Martial alisajiliwa na Man-United kutoka AS Monaco ya Ufaransa kwa Sh5.6 bilioni mnamo 2015. Ada hiyo ilimfanya Martial kuwa chipukizi ghali zaidi katika ulingo wa soka kwa wakati huo.

Tangu wakati huo, amefungia Man-United mabao 79 kutokana na mechi 268. Alipoteza uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha Man-United baada ya mabingwa hao mara 20 wa EPL kujinasia huduma za Cristiano Ronaldo, Edinson Cavani na Jadon Sancho.

Martial hajachezea Man-United katika mechi yoyote tangu Rangnick apokezwe mikoba ya kusimamia kikosi hicho na amewajibishwa mara 10 pekee kutokana na mashindano yote ya kikosi hicho msimu huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Arsenal waponda Norwich City na kumtia kocha Dean Smith...

Man-City wafungua mwanya wa alama sita kileleni mwa jedwali...

T L