Marufuku ndege za Afrika Ulaya

Marufuku ndege za Afrika Ulaya

Na AFP

SERIKALI za mataifa ya bara Ulaya mnamo Ijumaa ziliweka masharti ya kuzuia msambao wa aina mpya ya virusi vya corona, vilivyogunduliwa juzi nchini Afrika Kusini.

Kwanza, Uingereza na mataifa 27 wanachama wa Muungano wa Ulaya (EU), zilipiga marufuku ndege kutoka Afrika Kusini, Namibia, Zimbabwe, Botswana, Lesotho na Eswatini ili kuzuia msambao wa kirusi hicho kipya kwa jina Omicron.“Kuanzia Ijumaa saa sita usiku watu ambao sio raia wa Uingereza na jimbo la Ireland, hawataruhusiwa kuingia nchini humu ikiwa wamekuwa katika mataifa hayo sita ya kusini mwa Afrika siku 10 zilizopita.

“Raia yeyote wa Uingereza na Ireland watakaowasili kutoka mataifa hayo baada ya saa kumi alfajiri kuanzia Jumapili, sharti waende karantini kwa siku 10 kabla kuruhusiwa kutangamana na familia zao. “Waliowasili kabla ya siku hiyo sharti wazuiliwe nyumbani kwa siku 10,” akasema Waziri wa Afya wa Uingereza Sajid Javid.

Wanasayansi wa Uingereza, Afrika Kusini na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) wameelezea hofu kwamba aina hiyo ya kirusi ni hatari kuliko kile kingine cha Delta, kilichogunduliwa nchini India mapema mwaka huu.“Hii ni aina mpya ya virusi ambayo tumekumbana nayo wakati huu na utafiti wa dharura unaendelea kuelewa kasi ya msambao wake hatari, na ikiwa vinaweza kudhibitiwa kwa chanjo,” akasema Mkuu wa Shirika la Kupambana na Mradhi ya Kuambukiza nchini Uingereza, Jennie Harries, kwenye taarifa.

Katika siku za hivi karibuni, Ulaya imekuwa ikipambana na ongezeko la maambukizi ya Covid-19 huku idadi jumla ya watu waliofariki kutokana na ugonjwa huo ikipita 1.5 milioni.Kabla ya wanasayansi wa Afrika Kusini kuthibitisha uwepo wa aina hiyo mpya ya Covid-19, mataifa ya Uropa yalikuwa yakiendesha kampeni za utoaji chanjo kwa kulenga watu ambao hawajafikiwa.

Nchini Uholanzi serikali ilikuwa inajiandaa kukabiliana na wimbi la maandamano baada ya tangazo la Ijumaa la Waziri Mkuu Marka Rutte kwamba atafunga miji iliyoshuhudia visa vingi vya maambukizi.Kwa mfano, maafisa wa usalama walikabiliana na waandamanaji katika jiji la Rotterdam (lililoshuhudia idadi ya juu ya maambukizi mapya) Ijumaa jioni. Watu watano walijeruhiwa katika makabiliano hayo.

“Tumefungua macho na masikio yetu na tumeajiandaa kukabiliana na watu watakaozua fujo wakipinga mikakati ya serikali ya kudhibiti kuenea kwa Covid-19,” msemaji wa polisi jijini Rotterdam Gijs van Nimwegen akaambia AFP.Ujerumani, Jamhuri ya Czech na Ureno- ambazo zimeandikisha kiwango cha juu cha utoaji chanjo duniani- pia zilitangaza mikakati mpya ya kuzuia viwango vya maambukizi ya corona.

Chansela wa Ujerumani Angela Merkel alitoa onyo kali kwa serikali itakayochukua mamlaka akiitaka kuimarisha vita dhidi ya Covid-19 haswa msimu wa baridi unapokaribia.“Janga hili ni hatari na ninaomba serikali itakayochukua usukani kuwa macho,” akasema huku idadi ya waliofariki nchini humo kutokana na Covid-19 ikivuka 100,000.

You can share this post!

Gunners wakamatia chini Newcastle FC!

JAMVI: Roho ya Uhuru iko kwa OKA au Raila?

T L