Michezo

MaruFuku ya FIFA kuhusu Amrouche si mwisho wa dunia -FKF

April 23rd, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Soka la Kenya (FKF) limekata tamaa katika juhudi za kumlipa kocha wa zamani wa Harambee Stars, Adel Amrouche, na kwa sasa liko tayari kwa adhabu kali itakayotolewa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) dhidi yake.

FKF iliamrishwa na FIFA kumlipa Amrouche ambaye ni raia wa Algeria na Ubelgiji kima cha Sh109 milioni kwa kosa la kukiuka masharti ya mkataba wake alipotimuliwa mnamo Agosti 2014. Malipo hayo yalikuwa yawe yametolewa kufikia leo Alhamisi ya Aprili 23, 2020.

Hata hivyo, Rais wa FKF Nick Mwendwa, amesema kwamba wamejaribu kadri ya uwezo kulishughulikia suala hilo na wameshindwa kupata suluhu wala kuafikiana na wadau husika.

“Tumejaribu yote yaliyomo ndani ya uwezo wetu kuhakikisha kwamba tunamlipa Amrouche chini ya kipindi kilichoagizwa na FIFA. Yasikitisha kwamba tumeshindwa,” akatanguliza Mwendwa.

“Tumetalii njia na mbinu zote za kupata fedha hizo bila mafanikio. Tumeandikia FIFA ili itupatie muda zaidi wa kutafuta fedha hizo lakini sidhani kama watasikia kilio chetu. Tumejaribu pia kuhusisha serikali lakini kwa sasa inaelekeza juhudi zote katika vita vya kukabiliana na janga la corona. Haitawezekana kwa Amrouche kulipwa kabla ya leo (Alhamisi),” akasema.

“Hakuna lolote ambalo tunaweza kufanya kufikia siku ya makataa kwa sababu hatuna fedha zenyewe. Tunasalia sasa kusubiri maamuzi ya mwisho ya FIFA. Iwapo watatupiga marufuku ya kushiriki mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mnamo 2022, basi ni sawa. Haitakuwa mwisho wa dunia au maisha. Tutasubiri wakati mwingine, labda 2026 sasa,” akaongeza Mwendwa.

Iwapo FIFA itapiga Kenya marufuku, Mwendwa ameshikilia kwamba FKF itaelekeza juhudi zote katika harakati za kutambua na kukuza talanta za chipukizi kwa minajili ya mashindano mengine ya haiba katika ulingo wa soka kabla ya kuanza kujifua kwa fainali za Kombe la Dunia za 2026.

“Nawahakikishia Wakenya kwamba kupigwa marufuku na FIFA si mwisho wa dunia. Tuna mashindano mengi zaidi ya kushiriki mbele yetu. Mbani na Kombe la Afrika (AFCON) na CHAN, tuna mapambano ya haiba ambayo Harambee Starlets na chipukizi wetu wa vikosi vya U-17, U-20 na U-23 watashiriki katika kipindi hicho hicho cha kuandaliwa kwa mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar. Hivyo, sioni jambo hili likiwa pigo kubwa,” akasisitiza.

Mbali na uwezekano wa kupigwa faini, hatua dhahiri ambayo FIFA huenda ikachukua dhidi ya Kenya ni kuwatupa nje ya mechi za kutafuta tiketi za kuelekea Qatar mnamo 2022 sawa na jinsi Zimbabwe ilivyong’olewa kwenye michuano ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2018 nchini Urusi.

Chini ya kocha Francis Kimanzi, Harambee Stars kwa sasa wamo katika Kundi E pamoja na Mali, Uganda na Rwanda katika juhudi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022.

FIFA iliwapiga Zimbabwe marufuku ya kushiriki mchujo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2018 kwa kosa la kukiuka masharti ya kandarasi na kumnyima haki kocha mzawa wa Brazil, Jose Claudinei ‘Valinhos’ Georgino walipompiga kalamu mnamo Machi 2015.

Zaidi ya kutozwa faini, au (na) kupigwa marufuku, FIFA huenda ikaamua kuelekeza fedha za maendeleo ya soka ambazo Kenya hupokezwa kila mwaka kumlipa Amrouche huku FKF ikichukuliwa hatua kali za kisheria.